Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa (Mb), leo tarehe 20 Aprili 2025, ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kiruruma, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, kushiriki Ibada ya Sikukuu ya Pasaka.

Akizungumza mara baada ya Ibada hiyo, Bashungwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan kupitia kilimo cha mazao ya kimkakati kama kahawa.

"Rais Samia alipoingia madarakani alikuja na sera mpya na utaratibu wa minada ya kahawa kufanyika kupitia vyama vya msingi. Msimu uliopita tulishuhudia bei ya kihistoria ya kahawa. Na sasa, kwa mujibu wa mwongozo mpya wa Bodi ya Kahawa, msimu huu bei ya kuanzia kwenye mnada ni shilingi 5,000 kwa kilo, na ushindani wa bei unatarajiwa kuifanya ipande zaidi," amesema Bashungwa.

Ameongeza kuwa kupanda kwa bei ya kahawa kumesababisha ongezeko la vitendo vya wizi wa kahawa mashambani, hivyo amemuelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kuhakikisha Jeshi la Polisi linachukua hatua kali dhidi ya wahalifu hao.

“Nimeshamuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kuhakikisha Jeshi la Polisi linasimama imara kukabiliana na wezi wa kahawa ili wakulima waweze kunufaika ipasavyo na bei nzuri za zao hilo,” amesisitiza Bashungwa.

Katika Ibada hiyo iliyoongozwa na Paroko wa Parokia ya Kiruruma, Padre Cyril Ndamutahi, Mhe. Bashungwa ameanzisha harambee ya kuchangia ujenzi wa Makao ya Padre kwa kuchangia kiasi cha Shilingi milioni 10.

Awali, Padre Ndamutahi aliwahimiza waumini kuendelea kuwa karibu na Mungu kwa kushiriki ibada na shughuli mbalimbali za kanisa, akiwataka kuepuka mienendo inayowatenga na imani, ikiwemo uzembe wa kushiriki ibada na kutokujitoa katika kazi za kanisa.

Share To:

Post A Comment: