Dar es Salaam, Aprili 08, 2025 - Airtel Tanzania imewataka wateja wake kutoa taarifa mapema ili kuwafichua matapeli wa mtandaoni pindi wanapokutana na jumbe na kupigiwa simu na wahalifu hao wanaodai kuwa watoa huduma wa kampuni hiyo.

Kampuni hiyo imetoa wito huo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya utapeli ambapo serikali kupitia Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amekuwa akiwaomba wananchi kujikinga na kuwaficha watuhumiwa wa utapeli kwa njia ya simu za mkononi na kuzitaka kampuni za mawasiliano nchini kuongeza jitihada za kudhibiti utapeli kwa kuelimisha wateja wa mitandao hiyo.

Akizungumzia kuhusu hatua akiwa ofisini kwake makao makuu ya Airtel Tanzania, Mkurugenzi wa Mawasiliano na udhibiti wa kampuni hiyo, Beatrice Singano, alibainisha kuwa namba pekee ya watoa huduma ni 100 na kuwa nyinginezo ni majaribio ya matapeli ambao wanataka kufanya wizi wa taarifa na fedha kwa njia ya simu.

“Tunawaomba sana wasikubali kupigiwa simu na mtu yoyote ambaye atadai yeye ni wakala au mtoa huduma wa Airtel akiwapigia kwa namba nyingine yoyote isipokuwa 100. Lakini kama utakuwa umepigiwa na namba ya mtu ambae unahisi huyu ni tapeli basi tutakuomba utume hiyo namba kwa ujumbe mfupi kwenda 15040. Unaweza kutuma namba hiyo nasi tutaweza kuzipata taarifa hizo na kuhakikisha kwamba tunazifanyia kazi.

Singano alieleza zaidi kuwa watoa huduma wa Airtel Tanzania hawawezi kumpigia mteja kupitia namba nyingine huku akiwataka watumiaji wa mtandao huo kujihadhari na utapeli unaoweza kutokana na matumizi ya namba nyingine ambayo mteja anakuwa amesajiliwa kiholela.

“Tunaomba pia wateja whakikishe wanaangalia usajili wa namba zao kwa kupiga *106# na baada ya hapo watakutana na machaguo matatu; Chaguo la kwanza itakuambia uangalie usajili wako kama upo sahihi lakini ya pili itakuambia uangalie namba ulizozisajili. Lakini ya tatu itakuomba ufute namba ambazo huzijui. Hii ni muhimu sana kwa wateja wetu ili wajihadhari na uwezekano wa kuhusishwa na utapeli wa namba wasizozitambua,” alisema Singano.

“Mbali na hapo tunawaomba wateja kuwa pale wanapohisi wanakaribia kutapeliwa basi wahakikishe wanatambelea ofisi au maduka yetu yaliyopo sehemu mbalimbali nchi nzima. Tuna maduka zaidi ya 40 na matawi ya Airtel Money zaidi ya 2000 ambayo pia yanaweza kutoa msaada lakini tunaviosk vya Airtel Money ambavyo vinaweza pia kukuhudumia,” aliongeza.

Pamoja na hatua alizokwisha kuziainisha za kujikinga na uhalifu wa mtandao, Mkurugenzi huyo aliwataka wateja wa Airtel Tanzania kuhakikisha wanajenga desturi ya kuhakiki mawasiliano ya watu wao karibu ama marafiki pindi wanapopokea ujumbe wa kutuma fedha kutoka kwa namba za simu wasizozijua.

“Kumekuwa na utapeli mkubwa sana wa hizi message ambazo zinasema tuma hela kwenye namba hii au kuna mganga mahali anaweza kukusaidia shughuli zako mbalimbali. Kwa hiyo tunaomba sana wale ambao wanaokutana na hizo message nyingi na unakuta kwa bahati mbaya unakuwa na mtu ambae unataka kumtumia hela alafu ujumbe unaingia unasema tuma hela kwenye namba hii. Tunawasihi sana wateja wetu watakapoambiwa watume hela kwenye hela kwenye namba wasioifahamu tunawaomba kwanza wahakikishe wanacheki na muhusika kujiridhisha kama namba ni hiyo. Pia tunaomba wateja wetu wasikubali kupigiwa na watu kupitia namba ambayo sii namba 100,” alisema.
Share To:

Post A Comment: