NAIBU Waziri wa Madini, Dk, Steven Kiruswa amesema mkakati wa wizara hiyo ni kuhakikisha taasisi zake zinaelekeza nguvu katika mikoa yenye madini ya kimkakati ikiwemo kufanyiwa utafiti wa kina wa haraka ili kufikia asilimia 50 kabla ya mwaka 2030.
Aidha alisema mkakati wa wizara hiyo ni kupitia Dira 2030, yenye kauli mbiu ya madini ni maisha na utajiri itawezesha vijana wanaochimba madini kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuendelea kufanya utafiti kutoka asilimia 16 iliyopo sasa na kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka huo.
Hayo yalisemwa jana Jijini Arusha na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizaraya Madini
Alisema utafiti wa kina wa madini ukifanyika utawezesha ongezeko la fedha ikiwemo serikali kupata mapato sanjari na vijana wanaochimba madini kujikwamua kiuchumi kupitia sekta hiyo
"Lakini lazima pia tuhakikishe ongezeko la watumishi linakuwa ikiwemo kufanya utafiti wa madini kutoka asilimia 16 hadi kufikia 50 katika kuongeza pato la Haifa"
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini,Msafiri Mbibo alisema katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Februari, 2025 Wizara hiyo imepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa na kufikia asilimia 9.0 mwaka 2023 na kasi ya ukuaji kufikia asilimia 11.3 mwaka 2023.
Pia makusanyo ya maduhuli yanayowasilishwa hazina kwa kipindi cha Julai, 2024 hadi Februari, 2025 yameongezeka hadi kufikia sh, bilioni 690.76 ikilinganishwa na sh,486.30 katika kipindi kama hicho mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 42.04.
Alisema hivi sasa wanakamilisha utafiti maalumu na kuchora ramani Jiolojia ya visiwa vya Zanzibar (Unguja na Pemba) ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 wizara hiyo imejiwekea vipaumbele vya kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa sekta ya madini.
Huku Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi(TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Joseph Ngulumwa alisema mkutano huo unalengo wa kujadili wa bajeti 2025/26 ikiwemo kuipongeza Wizara ya Madini kwa kulipa madeni yote waliyokuwa wakidai watumishi hao mwaka 2023/24.
Pia waliomba watumishi upande wa masijali, waendesha ofisi watembelee migodi mikubwa ili kujua sekta ya madini jinsi inavyochangia pato la Taifa huku wakiomba kitengo cha manunuzi kuongezewa watumishi ili kuendana na kasi na ufanisi kazini.
Post A Comment: