Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kukamilika na kuzinduliwa kwa sera mpya ya ardhi ya mwaka 1995 toleo la mwaka 2023 kumehitimisha safari ya kushindwa kwa majaribio mengi ya marekebisho ya sera hiyo mpaka pale serikali ya Awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan ilipofanikisha kiu hiyo ya muda mrefu.
Wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa sera hiyo Mjini Dodoma leo Machi 17, 2025 mbele ya Mgeni rasmi Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Ndejembi amesema kwa mara ya kwanza mchakato huo ulianza mwaka 2010 kabla ya kufeli kwake na baadae jaribio jingine lilifanyika mwaka 2015 bila ya mafanikio kutokana na sababu mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza.
Akizungumzia safari hiyo, Waziri Ndejembi amesema kukwama kwa mapitio ya sera ya mwaka 1995 kulisababisha changamoto kadhaa ikiwemo kukithiri kwa migogoro ya ardhi pamoja na kuwa na sheria zisizoendana na wakati, suala ambalo limesababisha baadhi ya changamoto ikiwemo wanawake kushindwa kumiliki ardhi kisheria.
Kukamilika kwa sera hii chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kunatajwa kwenda sawia na mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia na kijamii sambamba na uzingatiaji mkubwa wa ukuaji wa kasi wa miji na idadi ya watu inayoshuhudiwa nchini, suala ambalo Waziri Ndejembi anasema kupitia maelekezo ya Rais Samia watahakikisha kuwa kufikia mwaka 2p3p ardhi yote inapimwa, kupangwa na kutambuliwa kwaajili ya maslahi ya kizazi kijacho.
Kauli mbiu kwenye uzinduzi huu wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 toleo la mwaka 2023 ni “ Sera ya Ardhi-Msingi wa Ustawi na Maendeleo Endelevu ya Taifa.”
Post A Comment: