Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam Awamu ya Nne (BRT 4) kuanzia Ubungo Daraja la Kijazi (Sam Nujoma) - Mwenge - Maktaba ya Taifa (Posta) yenye urefu wa kilometa 13.5. Na ujenzi wa miundombinu ya Mabasi hayo unaendelea kuanzia Mwenge hadi Tegeta (DAWASA) yenye urefu wa kilometa 15.63 ambapo ujenzi huo unatekelezwa na Wakandarasi wawili M/s China Geo Engineering na M/s Shandog Group Co. Ltd.
Akizungumza leo, Machi 5, 2025, katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Waziri Ulega amemkosoa vikali mkandarasi M/s China Geo Engineering kwa kuchelewesha kazi kinyume na makubaliano ya kimkataba ambapo amebaini kuwa licha ya kupokea malipo yote ya mradi huo, mkandarasi huyo bado ameonesha uzembe wa hali ya juu kwa kuwa na vifaa vichache, wafanyakazi wachache, na kupelekea kusababisha foleni kubwa jijini Dar es Salaam.
"Mkandarasi M/s China Geo Engineering anatuchezea, na wewe Mhandisi Mshauri unatazama! Kila mahali wamechimba, lakini hakuna zege. Kwanini mmebakiza mwezi mmoja wa kimkataba na bado mna mtambo mmoja wa kuzalisha zege?" alihoji kwa ukali Waziri Ulega.
Aidha, amemtaka mwakilishi wa M/s China Geo Engineering kuhakikisha mabosi wa kampuni hiyo wanawasili Tanzania kabla ya mwisho wa mwezi Machi, 2025 akisema kuwa Serikali haitasita kutumia njia za kidiplomasia kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa.
Aidha, wafanyakazi wa M/s China Geo Engineering wamelalamikia kutolipwa mishahara yao kwa wakati na kukosa marupurupu ya saa za ziada.
Kufuatia malalamiko hayo, Waziri Ulega ametoa agizo la haraka kwa mkandarasi kuhakikisha malipo hayo yanakamilika ndani ya saa mbili, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa endapo maagizo hayo hayatafuatwa.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Alois Matei, amesisitiza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Ulega yatafuatwa kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mabosi wa kampuni zinazotekeleza miradi ya BRT 4 Lot 1 na 2 wanawasili nchini kabla ya mwisho wa Machi.
Katika hitimisho lake, Waziri Ulega amewataka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na wahandisi washauri kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora na kwa wakati ili kupunguza kero ya msongamano jijini Dar es Salaam.
"Hatuna muda wa kuongezea mkandarasi siku za nyongeza! Watanzania wanapata adha kubwa ya foleni. Hakikisheni kazi inakamilika kwa muda uliopangwa, vinginevyo tutachukua hatua kali," alisisitiza Waziri Ulega.
Wakandarasi wawili M/s China Geo Engineering na M/s Shandog Group Co. Ltd wanaojenga barabara hizo, wamesema wamepokea maelekezo na Watayafanyia kazi huku M/s China Geo Engineering akiahidi kwamba atahikikisha Vifaa vyote vya Ujenzi vinafika Nchini Tanzania mwishoni mwa Mwezi Machi.
Kwa upande wa mradi wa upanuzi wa Barabara ya Morogoro, Waziri Ulega amekataa tarehe ya ukamilishaji ya Mei na Agosti 2025, akitaka kipande cha kwanza cha Kimara hadi Ubungo kikamilike ifikapo Aprili.
Post A Comment: