Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt. Stagomena Tax amewataka wanawake kuzitendea haki nafasi mbalimbali wanazozipata, akizitaka asasi za kiraia kutoa fursa sawa katika utendaji.

Dkt. Stagomena ametoa kauli hiyo katika ufunguzi wa kongamano la wanawake Kanda ya Kaskazini linaloendelea Jijini Arusha kuelekea siku ya wanawake duniani ambapo kitaifa yatafanyika Machi 08, 2025 ambapo mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye viwanja vya michezo vya sheikh Amri Abeid.

Waziri Tax pia ametoa wito kwa sekta binafsi kutoa fursa za hadhi na mazingira salama kazini kwa wanawake kwenye sekta ya utalii nchini, akihimiza pia jamii kupambana na ukatili wa kijinsia ambao mara nyingi umekuwa ukirudisha na kuwaacha nyuma wanawake kwenye maendeleo.

Waziri Stagomena kadhalika amehimiza wanawake kujiongeza na kutumia fursa mbalimbali zinazotengenezwa na serikali, akihimiza ushirikiano kati ya wanaume na wanawake katika nyanja zote, kwa kiwango sawa na malengo bora katika kufikia maendeleo ya wote.

Kwa upande wake Naibu waziri wa wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalum, Mwanaidi Ally Khamisi amesema kupitia kampeni ya Royal Tour, kumekuwepo na ongezeko la watalii, ukuaji wa pato la taifa na pato la mmoja mmoja.

"Wizara imeratibu kongamano hili ili kuhakikisha kila mshiriki anapata fursa sawa, na kwamba wanawake sasa wanatambua nguvu zao – ndiyo maana wanaongoza katika nyanja mbalimbali." Aliongezea

Hata hivyo Katibu Mkuu wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia na makundi maalum Dkt John Jingu amesema maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka huu 2025 yamepambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano ya kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Sambamba na hayo Jackline Mafuru ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wenye Makampuni ya Utalii Tanzania, ameonesha furaha yake kwa ukuaji wa sekta ya utalii ambayo imewajumuisha wanawake madereva, wapokezi, na hata waongozaji watalii, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa. Wajasiriamali walioshiriki kongamano hili wamesisitiza kuwa fursa hizo zinawafikia moja kwa moja, zikiwapa hamasa zaidi ya kupiga hatua mbele.



Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: