Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamadi Yussuf Masauni amesema wakati Tanzania ikiendelea kutatua changamoto za upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali inaongeza juhudi za ushirikiano wa kimataifa na kikanda ili kuondokana na vikwazo katika maeneo mbalimbali kama vile Mipango ya Kujenga Uwezo na Uhamasishaji, Utafiti, Ubunifu, na Maendeleo ya Teknolojia, Msaada wa Kifedha na Kiufundi, Ufuatiliaji, Tathmini, na Tathmini ya Athari.
Ameyasema hayo Machi 28, 2025 jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na balozi wa Finland nchini Tanzania Mhe. Balozi Theresa Zitting, Balozi wa Korea nchini Tanzania Mhe. Balozi Bi. Ahn Eunju pamoja na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Balozi Marianne Young. Mhe. Masauni amekutana na viongozi hao jijini Dar es Salaam Machi 28, 2025 ambapo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais (OMR) inakaribisha ushirikiano na wadau katika maeneo muhimu kama vile Mipango ya Mabadiliko ya Tabianchi na Kusaidia Utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupika (2024–2034).
“Ofisi ya Makamu wa Rais inahusika na masuala mawili, moja ni Uratibu wa Mambo ya Muungano, kwani utakumbuka kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili (Tanganyika na Zanzibar). Ofisi hii pia ina jukumu la uangalizi wa kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira na sheria, mikakati na vyombo vingine vya sera husika.Chini ya Ofisi hii, tuna taasisi mbili, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lenye jukumu la kuhakikisha uzingatiaji na utekelezwaji wa sheria na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) ambacho kina jukumu la kupima, kuhakiki na kutoa taarifa kuhusu utoaji wa gesi chafuzi katika viwango,” amesema Waziri Masauni.
Ameongeza Serikali ya Finland imekuwa ikisaidia uhifadhi kupitia Wizara ya Maliasili naUtalii, programu za misitu ya Mashamba; Programu za Kijiji cha Upandaji miti na kusaidia tasnia ya usindikaji wa kuni; Kujenga uwezo wa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni.
Mhe Masauni amesema Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupika (2024–2034) unaangazia upatikanaji wa suluhu za Nishati safi kwani bado kuna changamoto, ambapo zaidi ya asilimia 82 ya nishati ya msingi hutoka kwa mimea. Hivi sasa, karibu asilimia 90 ya kaya zinategemea kuni na mkaa kama nishati kuu ya kupikia, huku kuni zikichukua asilimia 63.5 na mkaa kwa asilimia 26.2 ya matumizi.
Pamoja na hayo wamezungumzia kuhusu Muhtasari wa Usimamizi wa Taka, ambapo amesema Tanzania inazalisha takriban tani milioni 14.4 hadi 20.7 za taka ngumu za manispaa kila mwaka, sawa na kilo 0.66 hadi 0.95 kwa kila mtu kwa siku au kilo 241 hadi 347 kwa mwaka.
Inakadiriwa kuwa 70% ya taka hizi zina vifaa vinavyoweza kutumika tena, lakini ni 5-10% tu ndio huchakatwa na sekta isiyo rasmi. Makadirio yanaonyesha kuwa kufikia 2030, karibu hekta 200 za ardhi zitahitajika kila mwaka ili kudhibiti tani milioni 26 za taka zinazozalishwa kila mwaka.
Kwa upande wake, Balozi wa Korea nchini Tanzania Mhe. Balozi Bi. Ahn Eunju amepongeza kwa juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Naye balozi wa Finland nchini Tanzania Mhe. Balozi Theresa Zitting kwa upande wake alizungumzia suala la Biashara ya Kaboni akieleza jitihada zinapaswa kuwekezwa zaidi eneo hilo, ambayo hapa nchini inaratibiwa na kituo cha NCMC kilichopo mkoani Morogoro.
“Eneo lingine ni kuhusu Uchumi wa Buluu hili pia ni sehemu nzuri ambalo nimeona kuna nguvu inafanywa na serikali kama ilivyo katika udhibiti wa taka na katika Nishati Safi hivyo nipende kuwapongeza,”
Pia Mhe. Masauni amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa lisilo la kiserikali la Good Neighbors ambapo walizungumzia kuhusu namna ya uboreshwaji wa Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira.
Post A Comment: