Naibu mkuu wa Chuo Fedha, Mipango na Utawala Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Grace Temba, amesema kuwa wanatambua mchango mkubwa wa viongozi wanawake na wanafunzi wa kike katika maendeleo endelevu ya chuo hicho.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la chuo hicho lililopo katika maonyesho yanayoendelea katika kuelekea siku ya wanawake Duniani ameeleza kuwa mafanikio ya chuo hicho yanatokana kwa kiasi kikubwa na mchango wa watumishi wanawake na kwamba chuo kitaendelea kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali ili kuwainua kiuchumi na kijamii.

Amebainisha kuwa chuo hicho kinaendelea kuwawezesha wanafunzi, hususani wa kike, kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na ubunifu wa biashara kupitia kiatamizi cha IAA Business Startup Centre (IBSUC), ili waweze kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.

Aidha, amewahimiza wanafunzi wa kike kutoogopa kusoma masomo ya sayansi na kutumia fursa zinazotolewa na chuo ili kuwawezesha kielimu na kiuchumi.

Hata hivyo kwa upande wake msimamizi wa kiatamizi cha IAA Business Startup Centre IBSUC, Sarah Mwaisumbo amesema wamefanikiwa kuwa na wanafunzi wajasiriamali zaidi ya 20, waliofanikiwa kuanzisha kampuni ambazo zinaendelea kufanya vizuri katika sekta mbalimbali za biashara, ambapo kupitia kiatamizi wanafunzi wanapata mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara, na mbinu za ubunifu ambazo zinawasaidia kuanzisha na kuendesha kampuni zao kwa ufanisi 

Rejoice Daniel ni Mwanafunzi wa diploma mwaka wa kwanza na mjasiriamali, ambaye yupo chini kiatamizi cha IBSUC ambapo ameshukuru chuo kwa kuwawezesha wanafunzi wa kike kupata nafasi ya mafunzo hayo kwa vitendo kupitia programu hiyo, na kwamba zinawasaidia wasichana kujitegemea kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii.

Siku ya kimataifa ya wanawake kwa mwaka huu inaongozwa na kaulimbiu isemayo " Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji"






Share To:

Post A Comment: