Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuendeleza rekodi nzuri ya makusanyo iliyowekwa kwa kipindi cha miezi nane mfululizo ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Akifungua kikao cha nne cha Baraza la Wafanyakazi wa TRA leo tarehe 04.03.2025 jijini Dodoma Kamishna Mkuu Mwenda amesema iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake TRA itaendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa Kodi.

Kamishna Mkuu Mwenda amewapongeza Watumishi wa TRA kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuimarisha uhusiano na Walipakodi ambao Imani yao kwa TRA imezidi kuongezeka na kuchochea ulipaji wa kodi kwa hiari.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema wapo baadhi ya Watumishi ambao wamekuwa wakilalamikiwa na Walipakodi kwa tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikichunguzwa kikamilifu na kuwahakikishia kuwa hakuna Mtumishi atayechukuliwa hatua kwa uonevu.

Amewataka kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuondoa malalamiko kutoka kwa baadhi ya Walipakodi.

Kamishna Mkuu Mwenda amewataka Watumishi hao kuendelea kuzingatia na kutekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi likiwemo agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan la kutaka kusimamia ulipaji wa Kodi kwa hiari.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema mbali na hayo Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kutoa maelekezo ya kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa na kuwachukulia hatua wale wanaojihusisha na ukwepaji wa Kodi kwa namna mbalimbali jambo ambalo linapaswa kusimamiwa na kila mmoja ndani ya TRA.

Amesema kufuatia maelekezo hayo na miongozo inayotolewa wameweza kuongeza makusanyo ya kodi na kuvuka malengo waliyowekewa na Serikali kwa miezi Saba mfululizo na kuwataka watumishi wa TRA kuendelea kuzingatia maelekezo hayo ili waendelee kuvunja rekodi ya makusanyo.

Kamisha Mkuu Mwenda ametaja miongoni mwa mambo yaliyowezesha kuvuka malengo kwa miezi Saba mfululizo kuwa ni pamoja na ulipaji wa Kodi wa Hiari unaohusisha utolewaji wa Elimu kwa Mlipakodi na ziara za Viongozi kuwafuata Walipakodi na kuwasikiliza hali ambayo imewezesha kutatuliwa papo kwa hapo kwa changamoto za Walipakodi.

“Pamoja na wenzangu ndani ya TRA wakiwemo mameneja wa mikoa tumekuwa na utaratibu wa kuwafuata Walipakodi na kuzungumza nao katika maeneo yao hii imetusaidia sana kutengeneza uhusiano wa karibu na Walipakodi, na Mimi binafsi nimepita mikoa yote na nimekutana na Walipakodi” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.

Amesema uhuru uliotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa TRA kufanya kazi zao bila kuingiliwa unapaswa kutumiwa ipasavyo kwa watumishi kujituma na kuhakikisha mianya yote ya ukwepaji kodi inazibwa hali ambayo itaendelea kuimarisha makusanyo ya kodi na kuleta usawa katika kukusanya Kodi.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema mapambano dhidi ya wakwepa Kodi yanapaswa kuongezeka ili kutowaumiza walipakodi waaminifu ambao wamekuwa wakifanya kazi zao katika sehemu moja na wasiolipa kodi jambo ambalo linapunguza ushindani wa kibiashara hali inayoweza kuua Biashara za Walipakodi waaminifu.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha amesema Baraza la Wafanyakazi ni chachu ya kuboresha utendaji kazi na kuwa kwa kipindi cha muda mfupi ambao Baraza hilo limekuwepo, manufaa yake yameonekana.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yahaya Kailembo amesema tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo miaka mitatu iliyopita wameweza kushughulikia changamoto mbalimbali za wafanyakazi na kuisaidia Mamlaka kutimiza wajibu wake. 

Kaulimbiu katika Mkutano huo wa Baraza la wafanyakazi wa TRA ni “Baraza la Wafanyakazi ni chachu ya utendaji kazi wenye tija, maadili na utumishi endelevu”






Share To:

Post A Comment: