Na Dixon Hussein .
Arusha – Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa
vitendo, wanawake wa Taasisi ya Utafiti wa Mboga Duniani (World Vegetable
Center) waliamua kupeleka elimu ya kilimo cha mboga kwa watoto wanaolelewa
katika kituo cha Matonyok kilichopo kata ya Olasiti, jijini Arusha.
Badala ya sherehe za kawaida, wanawake hawa waliamua kutumia
siku hiyo muhimu kuwapatia watoto ujuzi wa uandaaji wa shamba na uoteshaji wa
mboga, ili kuwasaidia kupata lishe bora na kuboresha afya zao. Mbali na elimu
hiyo, walitoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo mchele, sukari, sabuni, na
nguo, hatua iliyowafanya watoto hao kujihisi kupendwa na kuthaminiwa.
Mkurugenzi wa kituo cha Matonyok, Bi. Emmy Nicholaus Sitayo,
alieleza kuwa kituo hicho kilianzishwa mwaka 2006 kwa lengo la kuwahifadhi na
kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo wale waliokumbwa na
vitendo vya unyanyasaji kama vile ukatili wa kijinsia, kupigwa, na kunyimwa
haki zao za msingi. Hadi sasa, kituo hicho kinahudumia watoto 58, kati yao 30
wakiwa wasichana na 28 wavulana.
“Tunashukuru ujio wa wanawake wa World Vegetable Center, si
tu kwa msaada walioleta, bali kwa elimu ya kilimo cha mboga walichowapa watoto
wetu. Kupitia maarifa haya, watoto wataweza kupata mboga kwa chakula chao cha
kila siku na hatimaye kuwa na lishe bora inayosaidia kuimarisha kinga zao za
mwili,” alisema Bi. Sitayo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa World
Vegetable Center, Bi. Colleta Ndungulu, alisema kuwa wanawake wa taasisi hiyo
waliguswa na hali ya watoto wa Matonyok na waliamua kushiriki kwa vitendo
katika kuwapa ujuzi wa kujitegemea badala ya msaada wa muda mfupi.
“Tumeona ni muhimu kuwasaidia watoto hawa kwa kuwapa ujuzi
wa kilimo cha mboga ili waweze kujitegemea na kupata lishe bora. Hii ni sehemu
ya juhudi zetu za kuhakikisha kuwa jamii ina uelewa wa umuhimu wa mboga katika
afya na lishe,” alisema Bi. Colleta.
Mbali na uandaaji wa shamba na upandaji wa mboga, watoto hao
pia walifundishwa kuhusu makundi mbalimbali ya vyakula na umuhimu wa kula lishe
kamili. Mtafiti wa World Vegetable Center, Bi. Inviolate Mosha na Dkt Judith
Hurebert , aliwahimiza watoto hao kula mlo unaojumuisha vyakula vya aina zote,
ikiwemo nafaka, mizizi, nyama, samaki, maharage, na matunda, ili kujenga miili
yenye afya.
Watoto wa Matonyok walionyesha shukrani kwa fursa hiyo,
wakisema kuwa elimu waliyopewa itawasaidia si tu katika kituo chao, bali pia
katika maisha yao ya baadaye. “Sasa tunajua jinsi ya kupanda mboga na kuzitunza
hadi kuvuna. Tutakuwa na chakula chetu wenyewe,” alisema mmoja wa watoto kwa
furaha.
Hatua hii ya wanawake wa World Vegetable Center ni mfano wa jinsi taasisi na makundi mbalimbali yanaweza kushiriki kikamilifu katika kubadili maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Kwa kutumia Siku ya Wanawake Duniani kwa vitendo, wameleta mwanga mpya kwa watoto wa Matonyok, wakiwa na matumaini ya maisha yenye afya bora na ustawi endelevu.
Post A Comment: