Na. Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Mwanza
Serikali imewakumbusha wakopaji kusoma kwa kina masharti yote ya mikataba kabla ya kuchukua mikopo kutoka kwa Taasisi za kifedha ili kujiepusha na matatizo yanayoweza kutokea kutokana na masharti magumu au riba kubwa ambazo huathiri urejeshaji wa mkopo.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Arch. Chagu Nghoma, aliyasema hayo alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi zake ambayo imewasili mkoani humo kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa mkoa huo katika makundi mbalimbali.
“Tunaendelea kuwakumbusha wakopaji kuongeza umakini katika kusoma mikataba wanayoingia kutokana na kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa wakopaji ambao wanakabiliwa na riba kubwa, masharti magumu ya marejesho, na faini zisizoeleweka baada ya kushindwa kutimiza masharti ya mikopo.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa mkopaji ikiwa hajaelewa mkataba vizuri, atafute ushauri wa kisheria au wa kifedha kabla ya kutia saini mkataba wowote wa mkopo ili kujiepusha na matatizo yanayoweza kujitokeza baadae.
Arch. Chagu Nghoma, aliwasisitiza wakopaji kuwa waangalifu na kuepuka kukopa kwenye Taasisi za Fedha zisizo rasmi ambazo zinaweza kuwa na masharti kandamizi iwapo watashindwa kulipa mkopo.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, mkazi wa Buhongwa, Mwanza, Bi. Julieth Siange, alishukuru kwa elimu waliyoipata ikiwemo msisitizo waliopewa wa kutojiunga na vikundi ambavyo havijasajiliwa bali wajiunge katika vikundi rasmi vilivyosajiliwa na vinavyotambulika na Serikali ili matatizo yanapotokea waweze kusaidiwa kisheria.
Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa utoaji wa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa, pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuweka sheria na kanuni mbalimbali kwa watoa huduma za fedha jinsi wanavyotakiwa kuendesha Taasisi hizo, bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya watoa huduma kutofuata sheria na kanuni.
Bw. Kimaro, alifafanua kuwa kutokana na changamoto hizo kutoka kwa watoa huduma kutokuwa waaminifu, Serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na kuzichukulia hatua za kinidhamu ili kuhakikisha Taasisi hizo zinafanya kazi kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria.
Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi yote ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.
Post A Comment: