Na. Peter Haule, Tarime, Mara, WF.
Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro amewataka wakazi wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, kutoa taarifa kwa  Mamlaka husika inapobainika uwepo wa mtoa huduma ndogo za fedha asiyesajiliwa na anayetoa huduma kinyume cha Sheria.
 
Rai hiyo imetolewa wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha katika maeneo ya  Manga, Sirari, Matombo, Nyamwaga, Ganyange na Gorong’a, yaliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
 
Bw. Kimaro alisema kuwa uwepo wa watoa huduma ya fedha wasiosahihi wanachangia kwa kiasi kikubwa kufifisha maendeleo ya wananchi jambo ambalo Serikali haiwezi kulifumbia macho.
 
“Tumekuja kutoa elimu, tunafanya kwa jitihada kubwa kuhakikisha kwanza wananchi wanauelewa wa masuala ya fedha, wanatambua haki zao wakati wa kupata huduma za fedha na pia kuwa na uwezo wa kutambua huduma iliyosahihi na isiyosahihi ili waweze kuchukua hatua ikiwemo kupeleka taarifa katika Mamlaka husika pale inapobainika kunachangamoto ya watoa huduma hao”, alisema Bw. Kimaro.
 
Aidha, aliwataka wananchi kusimamia fedha zao na kuepuka kufanya sherehe au ngoma na mambo mengine yasiyokuwa ya maendeleo wanapopata fedha zinazotokana na shughuli zao halali za kiuchumu na badala yake wajiwekee akiba maeneo yenye tija kama vile Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja na Hati fungani za Serikali.
 
Bw. Kimaro alisema kuwa Utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 nchini, unaeleza kuwa ni asilimia 53.5 tu ya nguvukazi ndiyo waliotumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la Watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo na hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Alisema kuwa Programu ya Elimu ya Fedha kwa umma ilianza Mei, 2024, na hadi sasa mikoa 15 imefikiwa na uelekeo ni Mkoa wa Mwanza ambao anaamini watu wengi zaidi watajitokeza kupata elimu ya fedha kwa manufaa ya maisha yao.
Share To:

Post A Comment: