WACHIMBAJI wadogo wa madini wilayani Nyang’wale wameishukuru Serikali kwa  kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji ambao wanatoa msaada wa kiufundi ambapo elimu ya uchimbaji na vifaa vimetolewa kwa wachimbaji hao. Lengo ni kuwatoa kwenye uchimbaji mdogo na kuwa uchimbaji wa kati na baadaye mkubwa.

Akizungumza katika mahojiano, mmoja wa Wakurugenzi wa Mgodi wa Dhahabu wa  Igalula,  Jumanne Misungwi  amesema  mgodi huo ulipewa leseni mwaka 2019 lakini kulikuwa na changamoto za uzalishaji kutokana na kutokuwa na vifaa vya kisasa.

“Hatukuwa na teknolojia ya uzalishaji mwaka jana mwishoni tukaingia makubaliano na mwekezaji Zhong Tan Kun kwa utaratibu wa ‘Technical Support’, mfumo uliowekwa  na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan  kwa ajili ya kutusaidia wachimbaji wadogo, kwa sababu wao wana vifaa vingi, mkataba ni wa miaka mitatu,” amesema Misungwi,

Amesema tangu wawekezaji hao waanze kazi imetimia miezi saba, lakini miezi ya uzalishaji ni miwili mpaka sasa na kuongeza kuwa tayari wamezalisha  zaidi ya kilo 15 za dhahabu.

“Tunajivunia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wetu Anthony Mavunde, sisi wachimbaji hatuoni haya kusema  mitano tena,’’ amesema Misungwi na kuongeza,

“Waziri Mavunde tunajivunia nae sana amekuwa akishirikiana na sisi bega kwa bega kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini ya Mbogwe hakika tunaona manufaa ya uwekezaji.’’

Aidha, amesema kupitia uwekezaji katika mgodi huo wameweza kujenga Shule ya Sekondari inayofahamika kwa jina la Igalula Secondary-Gold Mine, ambayo imetokana na mgodi huo wa Igalula.

“Hii shule imetokana na mgodi wetu  sisi wazawa, sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa maabara katika shule hiyo.

"Kampuni imetoa ajira kwa wazawa, Rais Samia mitano tena. Uzalishaji ulikuwa mdogo kwakuwa mwamba wetu ni mlaini sana hautulii, haukuwa rafiki, wataalam kutoka Madini Mbogwe wakatushauri tuingie mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya msaada wa kiufundi ‘technical support’.

Kwa upande wa mwekezaji wa mgodi wa Igalula kutoka China, Liu Diheng amesema wameamua kuwekeza katika Sekta ya Madini Igalula kutokana na ushirikiano mkubwa wa kimahusiano uliopo kati ya Serikali ya China na Tanzania kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa China  Xi  Jinping  .

“Tumekuja kwa wingi kuwekeza Tanzania kutokana na historia ya kimahusiano iliyopo, tunawafundisha wazawa mbinu mbalimbali za kiufundi katika uchimbaji madini na vifaa, mwisho wa siku wananchi wa mataifa haya mawili, Tanzania na China wote tupate chochote kitu,”amesema Liu.

Nae, Juma Mashimba, Katibu Mkuu wa Kikundi cha Utulivu Mining Group  kilichopo kijiji cha Bululu Kata ya Nyamtukuza wilayani Nyang’wale Mbogwe mkoani Geita, amesema kikundi hicho kinaundwa na vikundi 16 vyenye wanachama 600 na walianza  uchimbaji mwaka 2019 lakini uchimbaji haukuwa na tija kutokana na ukosefu wa vifaa, ulikuwa umedorora ambapo hadi mwaka jana walikuwa wamezalisha kilogramu 9.7 pekee.

“Lakini mwaka 2024 mwishoni tukatafuta mwekezaji kampuni ya Zhongtan Longten Kuangye Mining ambaye tuliingia naye ubia kupitia utaratibu wa ‘technical support’

“Mchakato kidogo ulikuwa shida wachimbaji baadhi waligomea, Mheshimiwa Waziri Mavunde akaingilia kati  kutatua, mgogoro ukaisha tukaanza uzalishaji, mpaka sasa tumeshazalisha kilo 24 za dhahabu, tumelipa mrabaha wa Serikali zaidi ya milioni 280, TRA zaidi ya milioni 90 na halmashauri zaidi ya milioni 15,” amesema Mshimba.

Amesema, wamepata mafanikio makubwa tofauti na walivyokua wanachimba awali na kuendelea kufafanua,

“Tunashukuru Serikali kutuletea wawekezaji kama hawa angalau sasa kipato chetu kidogo kimeongezeka,”.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Kikundi cha Group 9 Mining Company Limited, Costatine Mazinzi amesema walipewa leseni ya uchimbaji Desemba mwaka 2019 ambapo awali walikuwa wanafanya uchimbaji mdogo wa maduara hivyo mwaka jana wakaingia mkataba na wawekezaji 'technical support' ili kuongezea maarifa ya uchimbaji, mkataba ni miaka mitatu ambapo mwishoni mwa mkataba wataweza kujisimamia wenyewe.

Aidha, amesema kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya ujenzi, kufikia mwezi Mei mwaka huu, wataanza uzalishaji,  ambapo matarajio yao ni kuzalisha si chini ya kilo 20 kwa mwaka.

















Share To:

Post A Comment: