Waziri wa Maji nchini Tanzania Mhe. Jumaa Aweso amewataka watanzania kumtunza, kumlinda na kumtumia vyema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujiletea maendeleo, akisema Rais aina ya Mhe. Samia Suluhu Hassan huwa hawapatikani kila wakati kote duniani.
Wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe leo Jumapili Machi 09, 2025 Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro, Waziri Aweso amesema kupitia upekee wa Rais Samia ndiyo umewezesha kuondoa adha kwa wanawake ya kutafuta maji umbali mrefu, akisema miradi zaidi ya 1000 inatekelezwa kote nchini katika kufanikisha dhamira njema ya Rais Samia.
Waziri Aweso amesema utekelezaji wa mradi huo haikuwa kazi rahisi, akikiri kuwa wapo waliofutwa kazi na wengine kulala Polisi, akitumia fursa hiyo kuwashukuru watendaji mbalimbali wa wizara hiyo kwa kufanikisha mradi huo akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara Bi. Mwajuma Waziri, ambaye Mhe. Aweso ameomba kumtangaza kuwa Mfanyakazi bora wa wizara kwa mwaka 2025 huku pia akimtangaza Injinia Emmanuel Maghembe kuwa Meneja ufundi wa mradi huo kutokana na utendaji wake mzuri wakati wa ujenzi wa mradi huo wa maji.
Mhe. Aweso amemuahidi Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa yeye pamoja na watendaji waliopo chini yake watahakikisha usiku na mchana wanashinda kwenye mradi huo ili kuhakikisha unakamilika na Maji kuwafikia wananchi, akipiga marufuku kwa Mamlaka zinazozimamia mradi huo kukata maji siku za mwisho wa Juma na nyakati za sikukuu.
Post A Comment: