Katibu wa Uchumi na fedha wa umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Happy Shirima amewataka vijana mkoani humo, kuepuka kutumika vibaya kisiasa na kujipanga vizuri na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu, ili kukihakikishia chama hicho ushindi wa kishindo.
Shirima ametoa rai hiyo, wakati wa kambi ya vijana zaidi ya 708 wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, inayofanyika katika Wilaya ya Hai mkoani humo, ambapo amesema ni wajibu wa vijana kukilinda chama hicho na kuhakikisha wanaepuka kurubuniwa ili wapatikane viongozi bora.
Amesema kama vijana wanapaswa kuepuka rushwa kwa kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali ili kujiongezea kipato na kuweza kusimama imara katika uchaguzi.
"Vijana tumejipanga vizuri na uchaguzi, lengo letu ni kuhakikisha CCM inashinda. Na Tunaweza kuepuka rushwa sisi kama vijana kwa kujituma vizuri katika kazi kujishughulisha na miradi ili kupata kipato chetu wenyewe na kujitegemea"
"Vijana tukiwa na kipato chetu hatutaweza kurubuniwa, tutasimama kifua mbele kupinga rushwa ya uchaguzi na kuwezesha kupatikana viongozi bora. Niwaombe vijana wenzangu tujipange vizuri"amesema Happy.
Aidha ametumia pia nafasi hiyo kuwataka vijana kujitokeza kugombea nafasi za ubunge na udiwani.
"Tayari Mgombea urais tunaye mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, lakini majimboni na kwenye kata baada ya bunge kuvunjwa kutakuwa wazi, niwaombe wakati ukifika tujitokeze kuchukua fomu".
Akizungumza Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Moshi vijijini, Yuvenal Shirima amesema kambi hiyo maalumu imewaandaa vyema kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.
"Tupo hapa Hai, kwa ajili ya kambi maalumu ya kimkakati kuelekea uchaguzi mkuu, kambi hii imelenga kufundisha vijana kujiandaa vizuri na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Kambi hii pia inawaandaa vijana kwenda kutafuta kura za kishindo za Rais Samia"amesema Yuvenal
Ameongeza kuwa "Katika kambi hii pia tumejifunza mambo ya kizalendo na masuala mbalimbali ya ulinzi na usalama kuelekea uchaguzi Mkuu. Lakini pia hii inatuwezesha kuendelea kukijenga chama na jumuiya zake ".
Post A Comment: