Katika jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika utafiti wa misitu na uhifadhi wa mazingira, ujumbe wa wanasayansi kutoka Urusi umetembelea Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Ziara hii ya siku mbili inalenga kuimarisha uhusiano wa kisayansi, kielimu na kiteknolojia kati ya Tanzania na Urusi katika sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira.
Wajumbe wa Urusi, wakiongozwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Ufundi wa Misitu cha Jimbo la Saint Petersburg, Chuo Kikuu cha Petrozavodsk, na Chuo Kikuu cha Misitu na Teknolojia cha Jimbo la Voronezh, walikutana na wenzao wa TAFORI kujadili maeneo ya utafiti wa pamoja. Katika mkutano huo, TAFORI iliwasilisha tafiti zake muhimu, ikibainisha fursa za kushirikiana katika nyanja za ikolojia, usimamizi wa misitu, na teknolojia za uhifadhi wa mazingira.
Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huu katika kutatua changamoto zinazokumba sekta ya misitu, kama vile mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya mimea, na matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya satelaiti na drones katika usimamizi wa misitu. Alisema, “Mashirikiano haya yanaleta pamoja wataalamu wa Tanzania na Urusi, na tutafaidika kupitia kubadilishana maarifa na uzoefu wa kisayansi.”
Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, alisema kwamba ziara hii itasaidia kuboresha juhudi za Tanzania katika utafiti wa misitu, hasa katika kukabiliana na changamoto za moto wa msituni na kuendeleza mbinu za kisasa za utafiti. Aliongeza kuwa, “Ushirikiano huu utatufundisha mbinu mpya na teknolojia zinazotumika Urusi, ambazo zinaweza kusaidia kuboresha uhifadhi wetu wa misitu.”
Watafiti kutoka Urusi wanajivunia mafanikio yao katika matumizi ya teknolojia za kisasa katika utafiti wa misitu, na walieleza kuwa wamefanikiwa kutumia teknolojia ya satelaiti na drones kutathmini hali ya misitu kwa ufanisi mkubwa. Pia, walisisitiza umuhimu wa utafiti wa pamoja katika maeneo ya uzalishaji wa miti bora, entomolojia, na usimamizi wa misitu kwa kutumia teknolojia ya AI.
Dr. Chelestino Peter Balama, Mtafiti Mkuu wa TAFORI, alitoa muhtasari wa mafanikio ya taasisi hiyo, akibainisha mchango wake katika juhudi za kimataifa za uhifadhi wa mazingira, pamoja na majukumu yake katika kulinda mimea inayo hatarini kutoweka. Alisema, “TAFORI ina nafasi muhimu katika utafiti wa misitu na mazingira, na ushirikiano huu na Urusi utaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na dunia kwa ujumla.”
Ziara hii imetia nanga kwenye ushirikiano wa kimasomo na kiteknolojia, ambapo pande zote mbili zitashirikiana katika kubadilishana wataalamu na kujifunza kutoka kwa kila mmoja. Vilevile, ufadhili wa masomo na miradi ya utafiti ya pamoja utasaidia katika kuboresha ufahamu wa kisayansi na kutatua changamoto za kimazingira.
Kwa kumalizia, Prof. Silayo aliwashukuru wataalamu wa Urusi kwa kutembelea Tanzania na kusema kuwa ushirikiano huu utaimarisha sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira, na kuleta tija kwa mataifa haya mawili. “Tunaamini kuwa kwa kushirikiana na Urusi, tutafanikiwa kutatua changamoto kubwa zinazokumba sekta yetu ya misitu,” alisema.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kisayansi kati ya mataifa, na inatarajiwa kuleta matokeo chanya katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya sekta ya misitu duniani.
Post A Comment: