Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 18, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.


Na Okuly Julius _DODOMA


Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ,Shirika la Viwango Tanzania (TBS),imepima sampuli 118,059 na kufanya ugezi wa vifaa 36,808 ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia sokoni zinakidhi viwango vya ubora.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 18, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.

"tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi mkubwa kwa lengo la kuhakikisha usalama wa bidhaa, kulinda afya za walaji na kuchochea biashara. Mafanikio haya yamepatikana kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, kuwezesha biashara, kuboresha mifumo ya TEHAMA, na kuimarisha maabara za Shirika, "amesema Dkt. Katunzi

Pia amesema ili kusogeza Huduma Karibu na Wateja
TBS imeanzisha ujenzi wa maabara mpya katika mikoa ya Dodoma na Mwanza ili kuhudumia wananchi wa Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa.

"Hatua hii itaongeza ufanisi wa huduma za uthibitishaji wa viwango kwa bidhaa za ndani na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa kutoka nje," alisema Mkurugenzi Mkuu wa TBS.

Aidha, shirika limetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kuimarisha ofisi zake saba za kanda pamoja na ofisi za mipakani. Lengo ni kuhakikisha bidhaa hafifu zinadhibitiwa kabla ya kuingia sokoni na kuhakikisha watumiaji wanapata bidhaa bora na salama.

Dkt. Katunza amesema katika miaka minne iliyopita, TBS imefanikiwa kuandaa viwango 1,823 katika sekta mbalimbali ikiwemo chakula, uhandisi, kemikali, na mazingira. Viwango hivi vinawasaidia wafanyabiashara na wazalishaji kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.


Pia, jumla ya leseni za ubora 2,402 zilitolewa kwa wazalishaji, ambapo kati ya hizo, 1,066 walikuwa wajasiriamali wadogo waliopata huduma bure kupitia mpango wa serikali.

"Serikali inatenga zaidi ya shilingi milioni 350 kila mwaka kusaidia wajasiriamali wadogo kupata nembo ya ubora bila malipo," alibainisha Mkurugenzi wa TBS.

Aidha, Dkt Katunzi ameongeza kuwa katika kuhakikisha bidhaa zinazosambazwa sokoni zinakidhi viwango, TBS imesajili jumla ya maeneo 31,592 ya uzalishaji, usambazaji, na uuzaji wa chakula na vipodozi. Shirika pia limekagua shehena 18,588 za bidhaa na magari 162,160 kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha bidhaa duni haziingii sokoni.

"TBS ina jukumu kubwa la kuhakikisha Tanzania haiwi jalala la bidhaa hafifu," alisema na kuongeza "Ukaguzi huu unalenga kulinda afya za wananchi na kuimarisha ulinzi wa mazingira."

ELIMU KWA WAZALISHAJI NA UMMA

TBS imeendesha mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa 5,052 ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango. Pia, kwa kushirikiana na SIDO kupitia Mradi wa Qualitan, shirika limefunza wazalishaji wa bidhaa za chakula 1,000 katika mikoa 10.

"Elimu ya viwango ni nyenzo muhimu kwa wazalishaji wetu ili waweze kushindana katika masoko ya ndani na nje," alisisitiza Dkt. Katunzi


KUONGEZA UFANISI WA MAABARA 


Maabara za TBS zimepata ithibati ya kimataifa na zina vifaa vya kisasa kama vile mashine ya hydrostatic pressure test, automatic conductor resistance tester, na solar simulator.

"Katika Afrika Mashariki na Kati, Tanzania ndiyo nchi pekee yenye mashine ya solar simulator, ambayo hupima paneli za jua bila kutegemea mwangaza wa jua wa moja kwa moja," amesema


MATUMIZI YA TEHAMA NA MFUMO WA DIRISHA MOJA 


TBS imeboresha mifumo yake ya TEHAMA kwa kuunganisha huduma zake na Mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (TeSWS).

"Mfumo huu unawawezesha wafanyabiashara kupata vibali na kuthibitisha ubora wa bidhaa kwa haraka zaidi," alisema mkurugenzi wa TEHAMA wa shirika hilo.


MKAKATI WA TAIFA WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA 

TBS inashiriki katika kuhakikisha vifaa vya nishati safi vinakidhi viwango vya kitaifa ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kulinda mazingira.

"Tunaendelea kununua vifaa vya kisasa vya maabara kwa ajili ya kuhakikisha vifaa vya nishati safi vinavyouzwa sokoni vina ubora wa hali ya juu," alisema mkurugenzi wa viwango wa shirika hilo.


TUZO NA ITHIBATI YA KIMATAIFA 


Mnamo mwaka 2023, TBS ilitunukiwa tuzo ya Mdhibiti Bora Barani Afrika kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Pia, TBS imekuwa taasisi ya kwanza katika SADC kupata ithibati ya mifumo ya udhibiti wa bidhaa kwa kiwango cha kimataifa.

"Tuzo hizi ni uthibitisho kuwa TBS inatekeleza majukumu yake kwa viwango vya kimataifa," alisema mkurugenzi mkuu wa shirika hilo.

TBS itaendelea kuweka mikakati ya kuboresha huduma zake kwa lengo la kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara nchini. Kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, Tanzania inazidi kujenga mazingira bora kwa wawekezaji, wafanyabiashara, na walaji wa ndani na nje ya nchi.

"Tunajivunia mafanikio haya na tunaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha bidhaa bora zinapatikana sokoni," alisema Mkurugenzi Mkuu wa TBS, "ameeleza Dkt. Katunzi
Share To:

Post A Comment: