Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mara ya kwanza imepokea Faru weupe 18 kutoka nchini Afrika Kusini kwa lengo la kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi,Dkt.Pindi Chana (Mb) ameyasema hayo leo katika hafla ya makabidhiano ya faru hao iliyofanyika katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mkoani Arusha leo Machi 4,2025.
"Mradi wa kupandikiza faru weupe ndani ya hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ni jitihada za kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini na unatekelezwa kwa mara ya kwanza kupitia makubaliano ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kampuni ya AndBeyond" amesema Mhe. Chana.
Mhe. Chana amefafanua kuwa katika makubaliano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kampuni ya AndBeyond ilichukua jukumu la kuwezesha upatikanaji na usafirishaji faru weupe 18 kutoka nchini Afrika Kusini kwa awamu ya kwanza na awamu ya pili inategemewa kupatikana kwa faru wengine 18 ili kufikisha jumla ya faru 16 ambapo wengine watawekwa katika maeneo mengine ya uhifadhi nchini.
Mhe. Chana amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihda za dhati za kukuza na kuimarisha sekta ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na mradi huo wa kupandikiza faru weupe.
Ameweka bayana kuwa Faru weupe ni moja ya wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka na hivyo kuorodheshwa kwenye makundi ya wanyamapori na mimea inayolindwa na Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo hatarini kutoweka (CITEs).
Kufuatia hatua hiyo amesema kiu ya Tanzania ni kuunga mkono juhudi za nchi nyingine hususan za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuwahifadhi wanyamapori hawa katika mazingira ya asili tofauti na maeneo mengine ambapo hufugwa katika mashamba maalum au bustani.
Amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine Faru weupe watatumika kutoa elimu kwa jamii juu ya usimamizi na uhifadhi wa faru, kuendeleza tafiti zitakazoleta matokeo yatakayoboresha sayansi na uhifadhi wa wanyama hao.
Kwa upande wake Kamishna Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dkt. Elirehema Doriye alisema kuwa kwa kupokea faru hao,Tanzania inathibitisha dhamira yake katika kuilinda spishi ya faru hao walio hatarini kutoweka.
"Faru hawa watachangia juhudi za kimataifa za uhifadhi wa faru, kutoa fursa za tafiti na kitaalamu, kuinua uchumi wa jamii, kukuza utalii na kwamba NCAA imejipanga kuwalinda na kuhakikisha usalama wao" amesema Dkt. Doriye.
Naye, Mwakilishi wa Viongozi wa Kimila kutoka Afrika Kusini, iNkosi Zwelinzima Gumedeunywano amesema kuwa lengo la kutoa Faru hao kwa Tanzania ni kuendeleza juhudi za Uhifadhi kwa kuongeza uzalishaji faru katika Afrika Mashariki.
"Tafiti zinaonyesha kwamba faru hawa watakua vizuri na kuzaliana katika eneo la Ngorongoro "amesema Bw. na kusisitiza kuwa wako tayari kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika juhudi za uhifadhi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Wadau wa Utalii kutoka kampuni ya AndBeyond nchini Afrika Kusini.
Post A Comment: