Na. Josephine Majura WF, Mara


Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Bi. Ainess Anderson, amezikaribisha Taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya fedha kwenda kutoa elimu ya fedha ikiwemo uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo kwa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

Alitoa wito huo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, Taasisi za Serikali na Binafsi kwa Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Tunawakaribisha muda wowote kuja kutoa elimu hii muhimu kwa watumishi na wakazi wa Halmashauri yetu ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha”, alisema Bi. Ainess.

Aliongeza kuwa Taasisi za Fedha zinatakiwa kuchangamka kutafuta wateja maeneo yote nchini hivyo wasikae ofisini hadi wakisikia Wizara ya Fedha inaenda kutoa elimu ndipo nao watoke ofisini waambatane nao.

“Wametoa mada nzuri ikiwemo aina za mikopo inayotolewa, vigezo vya kutambua Taasisi rasmi za kukopa, uwekaji wa akiba, kwakweli mada za leo zimetujengea  uelewa mpana wa masuala ya fedha, hivyo niwaombe na niwasisitize mrudi tena kwa wananchi wetu ili elimu hii nzuri kila mwananchi aipate iweze kumsaidia katika shughuli za kila siku za kiuchumi”, alisisitiza Bi. Ainess.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambae ni Mtumishi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Musoma, Bw. Juma Njwayo, ,alisema kuwa amepata elimu ya masuala ya fedha katika maeneo mbalimbali ikiwemo namna ya kuweka akiba, mikopo, Taasisi rasmi za kuchukulia mikopo na namna bora ya kujiandaa kabla ya kustaafu.

Kwa upande wake Afisa Msimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mzava, alisema kuwa katika mkoa wa Mara wamepata mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha.

“Tunaendelea kuwaomba wananchi tunapoendelea na zoezi la kutoa elimu ya fedha waendelee kujitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo  ili wawe na uelewa mpana wa masuala ya fedha”, alisema Bi. Elizabeth.

Katika zoezi la kutoa elimu kwa wananchi Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Fedha imeambata na Wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB na NBC.
Share To:

Post A Comment: