Na. Josephine Majura, WF, Ukerewe, Mwanza
Serikali imesema inatambua mchango mkubwa wa watoa huduma za kifedha nchini katika kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanapata fursa ya kufanya miamala ya kifedha kwa urahisi, hasa katika maeneo ambayo benki hazijafika.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, Mhe. Christopher Ngubiagai, alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambayo ipo mkoani Mwanza kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali.
Aliongeza kuwa watoa huduma za fedha wamekua na mchango katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kuwa kupitia watoa huduma hao wananchi wameweza kupata mikopo, kujiwekea akiba na kufanya malipo kwa njia za kidijitali.
“Serikali itaendelea kushirikiana na watoa huduma za fedha nchini ili kuhakikisha kuwa huduma hizi zinaimarishwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan waliopo vijijini na maeneo ya mbali.” Alisema Mhe. Ngubiagai.
Alifafanua kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na watoa huduma za fedha nchini, aliwataka kufuata sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha usalama wa mifumo ya kifedha, ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha na kukuza uaminifu katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Bw. Goodlucky Mtigandi, alisema mafunzo ya elimu ya fedha yamefika wakati muafaka kipindi ambacho wanashughulikia migogoro mbalimbali ya mikopo umiza.
“Tuamini mafunzo haya yatawasaidia wananchi kutambua umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha kwa maisha ya leo na kesho”, alisema Bw. Mtigandi.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, alizisisitiza Taasisi za Fedha zinazotoa mikopo kwa wananchi kuhakikisha wanarudisha dhamana kwa wakopaji mara tu wanapomaliza marejesho ya mikopo.
Akizungumza baada ya kupatiwa mafunzo ya fedha mmoja wa washiriki, ambaye ni Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Wilaya ya Ukerewe, Bw. Baraka Jeremiah, aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa mkopaji na mkopeshaji ili pande zote mbili zijue haki, wajibu na sheria zinazotakiwa kufuatwa.
Post A Comment: