Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema sera ya ardhi ya Mwaka 1995, toleo la mwaka 2023 itaimarisha na kukuza uwekezaji katika uendelezaji wa ardhi nchini kwa kuruhusu wageni na kampuni za kimataifa kuwekeza kwenye soko la ardhi ya Tanzania maarufu kama "Real Estate".

Wakati akizindua sera hiyo leo Jumatatu Machi 17, 2025 Jijini Dodoma, Rais Samia katika hotuba yake amesema sera iliyopita haikuruhusu uwekezaji huo kwa makampuni na raia wa kigeni, suala ambalo limelifanya shirika la nyumba la Taiga NHC kuzidiwa kutokana na mahitaji makubwa ya nyumba na makazi bora yanayotokana na kushuhudiwa kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini na hivyo kutekelezwa kwa sera hiyo mpya kunatajwa na Rais Samia kuwa kutavutia zaidi uwekezaji kutoka nje ya nchi.

Akiendelea kuzungumzia tija ya mapitio ya sera hiyo, Rais Samia amesema sera hiyo pia itaimarisha uthamini na ulipaji wa fidia za ardhi, kwa kuimarisha mfuko wa fidia kwa kuboresha upatikanaji wa haki kwa wakati na wenye kuzingatia thamani halisi ya ardhi husika, akiwataka watumishi wanaoratibu suala la fidia kubadilika na kuongeza weledi katika kusimamia utekelezaji wa sera hiyo.

Aidha Sera ya mwaka 1995, toleo la mwaka 2023 linatajwa pia kuimarisha fursa za uchumi wa buluu kwa kutoa usimamizi madhubuti wa rasilimali za kwenye maji katika kulinda manufaa endelevu ambapo sasa utafanyika upimaji wa ardhi iliyo chini ya maji ili kuwema alama na mipaka kwenye maziwa na bahari, katika kuepusha migogoro ya mipaka kati ya Tanzania na nchi za jirani.

Rais Samia vilevile amesisitiza kuwa misingi iliyowekwa kwenye sera ya mwaka 1995 haijabadilika ambapo umiliki wa ardhi umesalia kuwa wa mwananchi huku Rais akiwa ndiyo mdhamini Mkuu kwaniaba ya wananchi wote sambamba na ruhusa iliyowekwa sasa kisera ya kumruhusu mwanamke kuweza kumiliki ardhi na hivyo kuondokana na mila potofu zilizokuwepo awali kwenye jamii.
Share To:

Post A Comment: