Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Cuthbert Sendiga, mapema leo amepokea Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Justine Nyamoga, katika ofisi yake na kufanya kikao kifupi kabla ya kamati hiyo kuanza ziara yake ya kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Sekta ya Elimu kupitia program ya BOOST na SEQUIP, pamoja na miradi ya barabara inayosimamiwa na TARURA iliyotekelezwa kwa fedha za bajeti kwa mwaka wa fedha 2023\/24 katika mkoa wa Manyara. 

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Sendiga alisema kuwa Mkoa wa Manyara katika mwaka wa fedha 2023\/24 ulipokea jumla ya shilingi bilioni 70.9 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Sehemu kubwa ya fedha hizo ilielekezwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni, vyoo, pamoja na sekta ya afya hususan katika  ukarabati na ukamilishaji wa hospitali za wilaya, zahanati, na vituo vya afya.

Aidha, alieleza kuwa katika kipindi hicho TARURA walipokea jumla ya shilingi bilioni 11.79  kwa ajili ya  matengenezo ya barabara na vivuko.

Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa kupatikana kwa fedha hizi ni ishara ya dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha sekta za elimu, afya, utawala, na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

"Nichukue fursa hii kuishukuru Kamati ya Bunge ya TAMISEMI kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa ufanisi na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyotarajiwa," alisema Mhe. Sendiga.

Ziara ya Kamati ya Bunge ya TAMISEMI inatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Manyara ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa maelekezo stahiki kwa mamlaka husika.








Share To:

Post A Comment: