Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi kusimama kidete kuwashughulikia watendaji wa Wizara hiyo ambao wamekuwa kikwazo na sababu ya malalamiko mengi ya wananchi na hivyo kukwamisha dhamira njema ya kuwaletea wananchi ustawi.

Akizungumza wakati akizindua sera ya ardhi ya mwaka 1995 toleo la mwaka 2023, leo Machi 17, 2025 Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Rais Samia amesema sera hiyo imekuja na maboresho kadhaa katika kuondoa changamoto na malalamiko ya wananchi, hivyo mtendaji atakayekwamisha utekelezaji wake anapaswa kushughulikiwa kwani matarajio ya wananchi ni makubwa kwa serikali yao kupitia sera hiyo

Aidha Rais Samia ameelekeza katika kuimarisha usimamizi, upimaji, usajili na usimamizi wa ardhi nchini, ni muhimu Wizara kuupitia upya mfumo wake wa kiutendaji kwa kuangazia umuhimu wa kuwa na kamisheni ya ardhi itakayokuwa na majukumu ya kusimamia upimaji,ugawaji wa hati na usimamizi wa ardhi nchini Tanzania, huduma ambazo zitapatikana kwenye dirisha moja la huduma kwa mwananchi.

Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa Wizara kuendelea kuhakikisha kunakuwepo na nyumba za bei nafuu kwa wananchi sambamba na kufanya maboresho ya makazi kwenye miji na majiji mbalimbali akitolea mfano baadhi ya makazi duni yaliyopo kwenye maeneo ya Jiji la Dar Es salaam ikiwemo Mwananyamala na Kinondoni, akisisitiza umuhimu wa Majiji na Miji kuwa na hadhi na sura ya kuendana na Miji na Majiji.

Share To:

Post A Comment: