WAKATI Mfuko wa bima ya afya ukijivunia mafanikio makubwa ya Mfuko chini ya uongozi wa awamu ya sita, kwa kuongeza mapato na wigo wa kutoa huduma, pia umefanikiwa kuokoa zaidi ya bilioni 22 zilizotokana na udanganyifu wa utoaji huduma ya afya kupitia vituo vya afya huku ikivifungia vituo vya afya 11 nchini kutokana na udanganyifu huo.

Hayo yameelezwa leo Machi10 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa bima ya afya nchini, Dkt. Irene Isaka alipokuwa akielezea mafanikio ya utoaji huduma ya Mfuko huo katika uongozi wa awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Irene amesema ndani ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita, jumla ya matukio 229 ya udanganyifu yanaendelea kufanyiwa uchunguzi katika ngazi mbalimbali za kisheria nchini kutokana na udanganyifu huo huku kadi 13,000 zikiwa zimefungiwa kupata huduma ya afya kote nchini.

Hata hivyo amesema mafanikio yote hayo yametokana na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ambayo  inatumiwa na Mfuko huo katika awamu ya sita na kuondokana na mifumo wa kawaida.

Amesema katika kipindi hicho, watumishi 39 wameripotiwa kuhusika kwenye udanganyifu na walioonekana kuhusika moja kwa moja wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Dkt. Irene ametaja mafanikio mengine ya Mfuko huo ni pamoja na kuwa na ziada ya bilioni 95 za mapato hadi Disemba 2024. dhidi ya  nakisi ya bilioni 120 hapo awali hayo ni mafaniko ambayo yanatokana na kupunguzwa kwa gharama za uendeshaji, kubana matumizi na kukabiliana na udanganyifu.

“Napenda kuwaeleza tu kwamba hapo mwanzo Mfuko ulitetereka ulikuwa na uwezo wa kujiendesha kwa kipindi cha miezi 6 tu jambo ambalo ni hatari lakini hivi sasa Mfuko uwezo wa Mfuko umeboreka na unaweza kujiendesha kwa mwaka mmoja na miezi miwili  na tunataka kufikia uwezo wa kujiendesha miaka miwili kwa mujibu wa viwango vya kimataifa amesema na kuongeza:

“ Tumekuwa tukitumia mfumo wa kisasa wa kidijitali wa mawasiliano, yaani online system ambayo ni mfumo tunaotumia kufuatilia madai ya wabia na wagonjwa, mfumo huu umekuwa ukisaidia kuchakata madai na kuondoa udanganyifu, mfano unaumwa malaria lakini kituo cha afya umeandikiwa antibiotic mfumo unakataa kwa kuwa unatambua, mgonjwa wa malaria anatakiwa kunywa dawa gani,”anasema.

Amesema kwa kipindi cha miezi sita, Mfuko huo umefanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 384.20 na kusajili wanachama wapya 284,543 kipindi cha miezi sita. “ hii imesaidia kuongeza makusanyo hadi kufikia trilioni 2.3 katika kipindi cha uongozi wa awamu ya sita ambapo kati ya fedha hizo asilimia 92 zinatokana na makusanyo ya michango, asilimia 7 mapato ya uwekezaji na asimilia 1 vyanzo vingine.

Pia amesema ulipaji wa madai
 kwa vituo  vinavyotoa huduma kwa wanachama umeongezeka na hivyo kuongeza ubora wa huduma katika vituo hivyo vinavyotumia huduma ya NHIF kutokana na pato linalotoka katika Mfuko huo kuongezeka na kulipa kwa wakati tofauti na hapo mwanzo.

“ Tumeweza kulipa hospitali na vituo vya afya madai ya zaidi ya trilioni 2.29 ambayo ni sawa na asilimia 37 kwa hospitali za Serikali, asilimia 28 kwa hospitali za mashirika ya dini na asimilia 35 kwa hospitali binafsi,”amesema.

Amesema huduma za wazee yaani wastaafu zimeendelea kutolewa ambapo kwa kipindi cha mwaka jana, Mfuko huo umeweza kulipa hospitali zaidi ya bilioni 91 kwa kutoa huduma. Gharama hizo  zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Aidha ametoa wito kwa watanzania kubadilisha mfumo wa maisha kufuatia kuongezeka kwa wingi kwa wagonjwa wanaosumbuliwa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari ambayo yamekuwa yakiongeza gharama kubwa za matibabu kwa Mfuko huo.

Akizungumzia kuhusu waandishi wa habari kuungwa kwenye Mfuko huo Mkurugenzi huduma za Wanachama Hipoliti Lello amesema awali Mfuko huo ulitoa kifurushi maalum kwa wanahabari lakini walishindwa kutimiza vigezo na kutoa nafasi nyingine kwa umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), kukaa meza moja na Mfuko huo kuweka mikakati mipya ya namna wanahabari nchini wanaweza kufaidika na mpango wa serikali wa kupata bima ya afya kwa wote.

Amesema malengo ya baadae ya Mfuko huo ni kuongeza idadi kubwa ya wanachama kupitia sheria mpya ya bima  ya afya kwa wote ambapo ofisi yake imeanza mazungumzo na taasisi mbalimbali ili kuweza kuwaunganishaj watanzania kupitia makundi mbalimbali ikiwemo wakulima, wafugaji, wachimbaji madini wadogo wadogo .
Share To:

Post A Comment: