Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewataka
wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinadumu na kuwa bora zaidi.
Naibu Waziri Mahundi alitoa kauli hiyo tarehe 26 Machi, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya mawasiliano katika Jimbo la Tabora Kaskazini katika Kata ya Ifucha na kuongeza kuwa miradi ya mawasiliano inajengwa kwa gharama kubwa, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kushiriki katika kuitunza na kuilinda miundombinu hiyo dhidi ya uharibifu au wizi.
Naibu Waziri Mahundi amezitaka kampuni za simu kuhakikisha wanalipa walinzi wa minara ya mawasiliano kwa wakati ili kuongeza ari ya wafanyakazi hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
"Rais Dkt. Samia anapenda amani, na anapoleta miradi ya maendeleo kama hii, anapenda muitumie kwa amani," alisisitiza Naibu Waziri Mahundi.
Awali, akitoa taarifa kuhusu mnara huo, Kaimu Meneja wa Muko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bw. Shirikisho
Mpunji alisema kuwa mara huo ni miongoni mwa minara 758 ya mawasiliano inayojengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambapo Serikali imechangia shilingi milioni 109 kwa ajili ya ujenzi wa mnara huo unahudumia wakazi wa kijiji cha Kazima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kati, Bw. Saidi Iddy, alisema mnara huo ulianza kufanya kazi tangu Septemba 2024 na kwa sasa unahudumia wakazi wapatao 5,200 wa Kata ya Ifucha.
Post A Comment: