Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe kunatarajiwa kuwa na mchango katika kupunguza umaskini kwa Jamii kwa kutoa muda zaidi kwa wananchi kujishughulisha na uzalishaji mali badala ya kutumia muda mrefu kutafuta huduma ya Maji.

Aidha kukamilika kwa mradi huo pia utakaohudumia wananchi zaidi ya laki tatu kunatajwa kusaidia katika kuimarisha afya za wananchi wa Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kwani kutawaepusha wananchi na magonjwa mbalimbali ambayo yalikuwa yakitokana na matumizi ya maji yasiyokuwa safi na salama.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro wakati wa uzinduzi wa mradi huo leo Jumapili Machi 09, 2025, Rais Samia pia amesema mradi huo unatarajia kuvutia zaidi wawekezaji katika wilaya hizo za Same, Mwanga na Korogwe hasa kwa wawekezaji ambao. uzalishaji wa bidhaa zao umekuwa ukitegemea huduma ya maji.

Rais Samia amesema pia mradi huo utatoa fursa kwa wasichana kupata muda mrefu zaidi ya kujisomea na kutotumia muda mrefu kutafuta huduma ya maji kama ambavyo itarahisisha pia shughuli hizo kwa wanawake ambao sasa watapata muda zaidi wa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi.

Kukamilika kwa mradi huo kunawezesha upatikanaji wa maji ya uhakika wa lita Milioni 6 kutoka za awali za lita Milioni 3.7 kwa siku, ukitarajia kuhudumia wananchi takribani 300,000 kutoka 50, 615 wa awali sambamba na kutoa huduma hiyo kwa saa 24 bila mgao tofauti na awali ambapo huduma ya maji ilikuwa ikipatikana kwa saa sita pekee kwa siku.
















Share To:

Post A Comment: