Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti amesema Serikali imetoa mashamba ya kuzalishia mifugo ili kuwasaidia wafugaji kupata maeneo ya Malisho yatakayoongeza tija kwa uzalishaji wa mifugo bora na kuondoa migogoro baina ya Wafugaji na wakulima. 

Akizungumza mara baada ya kukagua mashamba ya kuzalishia mifugo Ranchi ya Kalambo iliyopo Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Machi 8, 2025 Mnyeti amesema Rais Samia Suluhu Hassan amechoka kusikia migogoro ya Ardhi baina ya wafugaji na wakulima hivyo serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itawanyang'anya watu wote waliopewa mashamba ya kuzalishia mifugo na badala yake kuyatumia kwa shughuli za kilimo. 

"Kwa ukubwa wa eneo hili ekari 150,000 tunauwezo wa kuleta ng'ombe wa Mtwara, Lindi tukawapa wafugaji vitalu vya ekari mia tano mia tano kwasababu tumechoka , Mhe. Rais amechoka migogoro ya wafugaji na wakulima" amesema Mhe. Mnyeti. 

Aidha Mhe.Mnyeti ameiagiza Kampuni ya Ranchi za Taifa ( NARCO) kuwandikia Notisi ya kuondoka kwenye mashamba ya kuzalishia mifugo wawekezaji walioshindwa kuyatumia mashamba hayo kwaajili ya mifugo na badala yake wamekuwa wakiyatumia kwa shughuli za kilimo jambo ambalo ni kinyume na mkataba wa upangishaji. 

Kwa upande wake Mwanasheria wa NARCO Saidi Seni amesma katika mkataba wa kuwapangisha wawekezaji hauruhusu shughuli za kilimo cha mazao tofauti na uzalishaji wa mifugo na malisho huku mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania( CCWT) Mrida Mshota akieleza hali ya uhitaji wa wafugaji wa mashamba hayo. 

Ranchi ya Kalambo inaukubwa wa hekta 64,650 zenye uwezo wa kuweka idadi ya ng'ombe zaidi ya 30,000 ambapo hadi kufikia mwezi Februari 2025 jumla ya hekta 29,465.96 zimekodishwa kwa wawekezaji wa mikataba ya muda mrefu ambayo ni miaka 33.

Share To:

Post A Comment: