

Naibu Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) - Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina akifungua kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa kuchunguza matokeo ya utumiaji wa teknolojia ya Blockchain katika kuongeza ubunifu jumuishi kwenye mnyororo wa ugavi wa kilimo Tanzania.
Mtafiti Mkuu wa mradi huo, Mhadhiri Mwandamizi (UDOM) Dkt. Hilda Mwangakala akielezea mradi wa kuchunguza matokeo ya utumiaji wa teknolojia ya 'Blockchain' katika kuongeza ubunifu jumuishi kwenye mnyororo wa ugavi wa kilimo Tanzania, wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi huo.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kwenye kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa kuchunguza matokeo ya utumiaji wa teknolojia ya Blockchain katika kuongeza ubunifu jumuishi kwenye mnyororo wa ugavi wa kilimo Tanzania.
Picha za pamoja kati ya viongozi na wajumbe walioshiriki kwenye kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa kuchunguza matokeo ya utumiaji wa teknolojia ya Blockchain katika kuongeza ubunifu jumuishi kwenye mnyororo wa ugavi wa kilimo Tanzania
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Naibu Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) - Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina amesema mradi wa kuchunguza matokeo ya utumiaji wa teknolojia ya 'Blockchain' katika kuongeza ubunifu jumuishi kwenye mnyororo wa ugavi wa kilimo Tanzania, utaenda kuwasaidia wakulima kufuatilia mwenendo wa soko la mazao.
Prof. Lokina ameyasema hayo leo Machi 18, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo na kuongeza kuwa kupitia mpango huo pia mkulima anaweza kufuatilia hali ya mazao yake yawapo ghalani.
"Hii itaenda kuondoa ile hali ya mnunuzi anakuja shambani anakuuliza una mikorosho mingapi, mnahesabiana ndipo ananunua. Sasa hiyo imeondoka, labda mtu atake mwenyewe kufanya hivyo. Kwa sasa unaweza kuvuna mwenyewe, ukapeleka kwenye ghala na kufuatilia mpaka mwisho," ameongeza Prof. Lokina.
Prof. Lokina amesema ni jukumu lao kama wanataaluma kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili waweze kupata faida.
"Ningetamani sana mfumo uweze kuonesha gharama ya kulima mkorosho mmoja mpaka kuvuna ni kiasi gani, ili unapopanga bei ujue hii inarudisha thamani yangu ya muda nilioutumia kwasababu mara nyingi huwa hatuangalii ule muda tulioutumia," amesisitiza.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa mradi huo, Mhadhiri Mwandamizi (UDOM) Dkt. Hilda Mwangakala amesema, mradi huo ni mwendelezo wa awamu ya kwanza ambayo walifanya mwaka 2022 kuanzia uliolenga kutafiti changamoto halisi wanazokutana nazo wakulima hasa wale wanaoshiriki mfumo wa stakabadhi ghalani na kilimo cha mkataba.
Dkt. Mwangakala amesema, baada ya kugundua changamoto hizo walibaini kwamba teknolojia ya 'Blockchain' inaweza kuzitatua, kwasababu ina sifa kubwa ambazo zitaongeza uwazi kwa kila mtu kwenye mnyororo wa ugavi kwani mkulima atakuwa na uwezo wa kuona taarifa na hakuna atakayeweza kuzibadilisha hizo kama wote hawajakubaliana kwenye mnyororo.
"Sasa malengo ya mradi yalikuwa kupitia sera ambazo zinaongoza mifumo hii miwili kwa maana ya mfumo wa skabadhi ghalani na mfumo wa kilimo cha mkataba, kwasababu tunaweza tukawa na suluhisho zuri au teknolojia nzuri lakini kama hakuna sera ambayo itawezesha utumiaji wa hii teknolojia bado ni changamoto," ameongeza.
Moja kati ya wakulima waliohudhuria katika kikao hicho Bi. Aisha Mwinyi amewashauri wakulima kupata elimu ya mkataba kabla ya kuingia kwenye makubaliano na wanunuzi kwani wengi wao wamekuwa wakiingia bila kujua maana yake na kupata mkanganyiko kwenye bei za mazao.
Post A Comment: