▪️Ampongeza Rais Samia kwa ujenzi wa miundombinu ya Elimu
▪️Aitaka jamii kuwakumbuka wenye mahitaji
▪️Akabidhi madaftari 10,000 kwa wanafunzi wenye uhitaji
▪️Shule sita zapata ufadhili wa ukarabati majengo
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde leo amegawa vifaa vya masomo ikiwemo madaftari 10,000 kwa watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu wa shule zote za Msingi ndani ya Dodoma Jiji.
Hafla hiyo imefanyika leo katika viwanja vya Shule ya Msingi Mazengo,ambayo ni shule aliyosoma Mbunge Mavunde,na kutanguliwa na ukaguzi wa miundombinu ya majengo ya madarasa na vyoo kisha katika tukio la kipekee Mbunge Mavunde amekutana na walimu wake wa darasa la Kwanza na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa kwake na kuwashukuru kwa kuwachangia Bima ya Afya ya Tsh 7.4m.
“Tunaishukuru serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu Jijini Dodoma huku tukishuhudia ujenzi wa shule mpya 12 za msingi ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu.
Katika kuendelea kuboresha mazingira rafiki ya kusoma,leo nitakabidhi madaftari 10,000 kwa watoto yatima na wale waishio mazingira magumu.
Aidha,tumepata ushirikiano na Taasisi ya Msaada wa Elimu iliyopo nje ya nchi ambao wameonesha nia ya kufanya ukarabati mkubwa wa shule sita za Jijini Dodoma ikiwemo shule ya Msingi Mazengo ambapo kwa kuanzia nitachangia matofali 5000 na kushawishi wanafunzi wengine waliosoma hapa kuchangia kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule”Alisema Mavunde
Wakitoa salamu zao Diwani wa Kata ya Kikuyu Kaskazini Mh. Israel Mwansasu na Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi Mwl. Prisca Myalla wamempongeza Mbunge Mavunde kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuimarisha sekta ya Elimu Dodoma Jiji na kuboresha mazingira ya kujifunza kwa wanafunzi.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazengo Mwl. Rehema Nkungu amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kujali watoto wahitaji na kwa kusaidia maendeleo makubwa ya shule hiyo kupitia michango mbalimbali ambayo imeboresha mazingira ya kujifunzia.
Post A Comment: