Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla ameendelea kukipiga mkwara chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nakusema ajenda yao ya No reform no election ianzie ndani ya chama chao.
Amesema Mwenyekiti wa Chama hicho Tundu Lissu wakati anaomba wanachama wa mchague kushika wadhifa huo aliahidi kufanya mabadiliko makubwa ikiwemo kuweka ukomo wa uongozi lakini baada ya kuingia amekaa kimya.
Msingi wa hoja ya Makalla amedai mabadiliko ya mifumo huru ya uchaguzi inayoshinikizwa na Chadema haina tija yeyote kwani tayari imeshafanyika ikiwemo wakurugenzi kutokusimamka uchaguzi na hakuna mgombea atakayeshinda bila kupingwa.
Akizungumza kwenye muendelezo wa ziara zake anazozifanya katika wilaya za mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanya mkutano ya ndani na viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya shina hadi wilaya kuhimiza watanzania kujitokeza kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura.
Akiwa kwenye mkutano wa ndani uliofanyika viwanja vya Toto Tundu Kata ya Tabata Segerea, Makalla amesema anashangaa kuona chama hicho kuja na ajenda hiyo na kudai watazuia uchaguzi.
"Niwaambie hizo no reform no election wanazosema zianzie kwanza ndani ya chama chao, mbona wakati anapoga kampeni kugombea nafasi ya uenyekiti wa Chadema alikuwa anasema Freeman Mbowe amekaa muda mrefu na kuahidi akiingia atafanya mabadiliko.
"Baada ya kuingia amekaa kimya wala hazungumzi chochote, nasema ajenda hiyo ianzie kwanza kwenye chama chao," amesema.
Makalla amesema hata kampeni wanayoendesha kutaka kuzuia uchaguzi kwa nguvu ya umma haiwezi kufanikiwa kwani CCM kina umma mkubwa kuliko Chadema.
"Kuzuia uchaguzi uliopo kwa mujibu wa sheria ni kosa kubwa, kwanza niseme hawawezi kufanikiwa na wasipo shiriki uchaguzi suala la kuitwa chama kikubwa cha upinzani litakuwa limeisha," amesema
Kulingana na Makalla ambaye ni mlezi kwa mkoa huo, amesema anachokiona Chadema iwapo hawatashiriki uchaguzi wanataka kuua ndoto za waliotamani kugombea nafasi mbalimbali za udiwani na ubunge.
"Chadema wanasumbuliwa na bundi na wanajaribu kuzungumza ajenda hii kutaka kuziba mgawanyiko unaoendelee ndani ya chama hicho kutokana na uchaguzi wa ndani walioufanya," amesema
Post A Comment: