Na WAF, ARUSHA 

Tanzania  imepunguza maambukizi mapya ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia 40 hatua inayoiweka nchi katika mwelekeo sahihi wa kufanikisha lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani jijini Arusha, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya, hususanni miundombinu, vifaa tiba na upatikanaji wa dawa.

"Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeimarisha mfumo wa huduma za afya kwa kuongeza vituo vya uchunguzi, kuboresha vifaa tiba na kuhakikisha upatikanaji wa dawa za Kifua Kikuu, hatua ambazo zimeleta matokeo chanya na kupunguza vifo na maambukizi," amesema Dkt. Mollel.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka wagonjwa 308 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000 mwaka 2024. Vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu pia vimepungua kwa asilimia 68, kutoka vifo 58,000 mwaka 2015 hadi vifo 18,400 mwaka 2024.

Kwa upande wake, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma, Dkt. Riziki Kisonga, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya afya na jamii ili kuzidisha mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.

Amesema jitihada za Serikali zinalenga kuhakikisha wagonjwa wanagunduliwa mapema na kuanzishiwa matibabu ili kupunguza kusambaa kwa ugonjwa huo.

"Tunahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa Kifua Kikuu mapema, kwani kugundua ugonjwa huu katika hatua za awali inasaidia matibabu kuwa na ufanisi zaidi na kupunguza hatari ya maambukizi kwa wengine," amesema Dkt. Kisonga.

Katika kukabiliana na changamoto zinazoendelea, Wizara ya Afya imeanzisha kampeni maalum katika Halmashauri 76 zilizopo katika mikoa tisa, kampeni ambayo hadi sasa imewezesha kugundulika na kuanza matibabu kwa wagonjwa 9,585 wa Kifua Kikuu. Serikali pia imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa dawa na huduma bila malipo licha ya changamoto za ufadhili kutoka kwa baadhi ya wahisani wa kimataifa.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu “Kwa Pamoja Tunaweza Kutokomeza Kifua Kikuu: Azimia, Wekeza, Timiza”, ikihimiza mshikamano wa sekta zote kwenye kutokomeza ugonjwa huo.

Share To:

Post A Comment: