Na. Saidina Msangi, WF, Mwanza.

Serikali imewasisitiza Maafisa Masuuli nchini kuhakikisha kuwa Taarifa za Mali zote za Umma, zinaingizwa na kutunzwa kwenye mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali za Serikali na taarifa husika zinatumika kwenye kufunga hesabu kwa mwaka 2024/2025.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu mkoa wa Mwanza, Bw. Chagu Ng’oma, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, anayesimamia Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Christian Omolo, wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Mali za Serikali kwa Maafisa Masuuli wa Taasisi za Umma 106 ikijumuisha Halmashauri 58, yaliyofanyika katika ukumbi wa TMDA, jijini Mwanza.

Alisema kuwa Wizara ya Fedha imeongeza ufanisi wa Usimamizi wa Mali za umma nchini kwa kusimika na kuwezesha matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali za Serikali “Government Assets Management Information Systems - (GAMIS) ambao unatumika kutunza na kuchakata taarifa za mali za Taasisi zote za Umma hapa nchini.

‘‘Nasisitiza kutumia mfumo wetu wa GAMIS kutunza taarifa za mali za umma lakini pia taarifa husika zitumike kwenye kufunga hesabu kwa mwaka 2024/2025 kulingana na Waraka Na. 2 wa Hazina wa mwaka 2021/2022, ili kupunguza hoja zinazobainishwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa taasisi mbalimbali za umma’’, alisema Bw. Ng’oma.

Aidha, alielekeza kuwa mali za umma ambazo ni chakavu, sinzia, ziada na zilizokwisha matumizi zinaondoshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo kufikia tarehe 30 Juni, 2025.

Bw. Ng’oma alisema kuwa ni muhimu kuhakikisha kuwa mali za umma zinatunzwa, kufanyiwa matengenezo stahiki kwa wakati na zinatumika kwa manufaa ya Umma.

‘‘Serikali inatumia fedha nyingi katika upatikanaji na utunzaji wa rasilimali inatupa kila sababu ya kuwa na mikakati madhubuti ya kuzisimamia mali hizo ili ziweze kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuiwezesha Serikali kupata manufaa ya uwekezaji uliokusudiwa kwa kipindi kirefu’’, alisema Bw. Ng’oma. 

Aidha, Bw. Ng’oma alielekeza kuwa Maafisa Masuuli wasimamie na kuhakikisha kuwa mali za miradi zinakabidhiwa kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali mara baada ya miradi husika kufikia ukomo.

Alisema Maafisa Masuuli wanabeba jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa mali za umma zinatumika kwa matumizi yaliyopangwa na kwa manufaa yaliyokusudiwa, hivyo uwajibikaji, uwazi, na ufanisi ni misingi muhimu katika kuhakikisha kwamba, mali za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Wizara ya Fedha Bw. Ismael Ogaga, alisema kuwa Wizara ya Fedha ina jukumu la usimamizi wa mali za umma nchini na kutokana na jukumu hilo na changamoto nyingi katika eneo la usimamizi wa mali, imeandaa mafunzo kwa Wakuu wa Taasisi kuwajengea uwezo ili waweze kusimamia vema mali zilizo chini ya usimamizi wao.

‘‘Baada ya mafunzo haya ni matumaini yetu kuwa mtapata uelewa wa kutosha wa namna bora ya kusimamia mali za Serikali kwa manufaa ya umma kwa muda mrefu, niwashukuru sana kwa ushiriki wenu katika mafunzo haya na tunatarajia mtafanyia kazi yale mliyoyapata kutoka kwenye mafunzo haya’’, alisema Bw. Ogaga.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Bi. Aines Anderson, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuendesha mafunzo hayo kwani yatawawezesha kuimarisha utendaji kazi ikiwemo matumizi sahihi ya mfumo wa GAMIS mbao utawawezesha kupunguza hoja za CAG.

Mafunzo hayo yaliyohusisha Maafisa Masuuli kutoka Halmashauri 58 zilizoko katika Mikoa nane (8) ya Mwanza, Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Mara, Simiyu na Kigoma, yalilenga kuwajengea uwezo washiriki juu ya sheria, kanuni na miongozi inayohusu masuala ya usimizi wa mali za Serikali ili kupunguza hoja za ukaguzi zinazotolewa kwa Taasisi za umma na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Share To:

Post A Comment: