Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amehitimisha kilele cha Maadhimisho ya siku ya Mwanamke Duniani Kimkoa leo Machi 6, 2025 yaliyofanyika kwenye Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Ametoa wito kwa wanawake wote kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata elimu kwani elimu ndiyo msingi wa maisha bora kwa jamii na kwa Taifa.
Mhe. Macha amewataka wanawake kuchangamkia fursa za mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri ikiwa na Lengo la kuwainua kiuchumi kuliko kukimbilia mikopo ya kausha damu inayotolewa kwa masharti magumu pamoja na riba kubwa inayopelekea kudidimia kiuchumi.
Aidha amewasihi wanawake kuendelea kutumia nishati safi kwa mazingira ikiwa ni pamoja na matumizi ya gesi na mkaa bandia unao tengenezwa viwandani kwa kutumia mabaki ya pumba za Mpunga kwa ajili ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Mazingira yanabaki salama.
Mhe. Macha amekabidhi hundi zenye jumla ya thamani ya Sh. 1,508,915,000/= kwa Halmashauri tatu ikiwa Msalala sh. 317,255,000/=, Shinyanga Vijijini sh. 152,500,000/= na Ushetu sh. 1,039,160,000/= na kuwataka wanufaikaika hao kuitumia vyema mikopo hiyo kwani si mali yao bali ni fedha za Watanzania wote ambazo zitatakiwa kurejeshwa kusudi na wengine wapate kunufaika.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Mhe. Salum Hamduni amewashukuru wananchi na wadau wote waliojitokeza kushiriki katika Maadhimisho hayo na kuwataka kuendelea kufanya jitihada kuhakikisha maslahi ya mtoto wa kike yanaendelea kulindwa na kuboreshwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bi. Rose Manumba amewataka wanawake kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anapambana Kuhakikisha maendelea yanapatikana katika Taifa letu na huduma bora na nzuri kuendelea kupatikana kwa kina Mama.
Maadhimisho haya yamefanyika kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia Machi 4 na kufikia kilele chake Machi 6, 2025 katika Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Kauli Mbiu “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”.
Imewasilishwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Msalala, DC.
![]() |
Post A Comment: