Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesisitiza umuhimu wa Mkoa wa Tanga katika sekta ya nishati, akisema kuwa ni kitovu cha kupokea na kusambaza mafuta kwa mikoa ya Kaskazini.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kituo cha gesi cha GBP Tanga leo Jumamosi Machi Mosi, 2025, Kapinga ametaja ushirikiano wa kiuchumi na wawekezaji wa GBP kama muhimu katika kukuza sekta ya nishati, hususan katika mafuta na gesi.
Kapinga amesema kwamba, kupitia sera nzuri za uwekezaji zinazotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imekuwa kivutio kwa wawekezaji, hasa katika sekta ya nishati safi ya kupikia.
Amesema, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imekuwa ikisapoti wawekezaji kwa kutoa afua za kikodi ambazo zinahamasisha uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kutoa msukumo kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya LPG na vifaa vinavyohusiana na uzalishaji wa nishati safi.
"Serikali imekuwa ikitekeleza sera zinazowezesha wawekezaji kushindana na wenzao kutoka nje ya nchi, na hii inatokana na msukumo wa soko katika nishati safi ya kupikia," alisema Kapinga.
Aidha, Naibu Waziri amesisitiza kwamba pamoja na uwezo wa nchi kuhifadhi tani 15,700 za gesi, uwekezaji wa GBP na wengine kama hao wa Chongoleani na Dar es Salaam unazidi kuimarisha sekta ya mafuta na gesi nchini.
Kapinga amekiri juhudi za Rais Samia katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia, akisema kuwa lengo la asilimia 75 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2030 lipo njiani kutimia kwa mafanikio makubwa, akiongeza kuwa sekta ya nishati inazidi kupata msukumo mkubwa kutokana na sera bora zinazotekelezwa na Serikali.
Post A Comment: