Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. David Mathayo David, imeanza ziara yake mkoani Njombe kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati na madini.

Kamati hiyo imepokea taarifa ya utekelezaji wa miradi usambazaji umeme vijijini kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Taarifa hiyo imesomwa na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi sasa zaidi ya asilimia 98 ya vijiji mkoani Njombe vimeunganishwa na umeme kupitia miradi mbalimbali ya Turnkey Awamu ya kwanza ya pili na ya tatu, huku maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Vitongoji Awamu ya Pili B yakiwa ukingoni.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. David Mathayo David, amepongeza juhudi za serikali katika kusambaza umeme vijijini na kusisitiza umuhimu wa kukamilisha vijiji vilivyosalia kwa wakati.

"Umeme vijijini ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika sekta mbalimbali kama kilimo, biashara, afya, na elimu. Tunaitaka TANESCO na REA kuhakikisha wanakamilisha miradi hii kwa wakati ili wananchi wanufaike ipasavyo," alisema.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa miradi ya umeme vijijini imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya wananchi, hasa katika sekta za uzalishaji na huduma za jamii.

Katika ziara hiyo, Kamati ya Bunge itatembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA katika mkoa wa Njombe.




Share To:

Post A Comment: