Na Denis Chambi, Tanga.
BONDIA wa Ngumi za Kulipwa hapa nchini na bingwa wa mkanda wa WBO Afrika Hassan Mwakinyo anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kwa tuhuma za kumshambulia Mussa Ally kwa kile kilichodaiwa kwa aliingia katika makazi ya bondia huyo bila ridhaa yake
Akizungumza na vyombo vya habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius Mchunguzi ameeleza kuwa uchunguzi wa shauri hilo unaendelea mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linamshikilia Hassan Mwakinyo mwenye umri wa miaka 29 mkazi wa Sahare jijini Tanga kwa tuhuma za kumjeruhi na kumshambulia Mussa Ally (21) huyu ni mvuvi mkazi wa Sahare uchunguzi wa shauri hili unaendelea ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria"
Kamanda Mchunguzi abainisha kuwa baada ya kufanya mahojiano na Mtuhumiwa (Mwakinyo) alidai kuwa Mussa Ally ambaye aliingia katika eneo lake alimchukulia kama ni mwizi huku Jeshi hilo likiendelea kuchunguza madai ya wananchi ambao wamemtaja Bondia huyo kuwa na tabia ya kuwashabulia baadhi yao pasipo sababu.
"Baada ya kuhojiwa yeye alieleza kuwa yule mtu alimchukulia kama ni mwizi lakini kumhisi mtu kama ni mwizi hakukupi mamlaka ya kuchukua Sheria mkononi na ndio maana Jeshi la Polisi limemkamata na kuendelea kuchunguza kuwa ni kipi kiini cha kumshambulia huyu mhanga ambaye alipata tatizo hilo"
"Ni kweli kuwa kumekuwepo na tuhuma mbalimbali ambazo zinamtuhumu Hassan Mwakinyo kwamba amekuwa akifanya vitendo kama hivi siku za nyuma Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi na kama mtu yeyote ana taarifa ya tuhuma hizo alete Jeshi la Polisi litashughulikia" alieleza Kamanda huyo.
Kufwatia tukio hilo Kamanda Mchunguzi amewaasa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia Sheria mkononi badala yake kutoa taarifa kwenye vyombo vya Sheria pale wanapoona matukio ya uhalifu na wahalifu vinginevyo watajikuta wanajiingiza kwenye makosa ya jinai.
Akizungumza kijana Mussa Ally ambaye ndiye aliyejeruhiwa na katika tukio hilo alieleza kuwa March 4 ,2025 majira ya saa 11 Alfajiri akiwa anapita njiani karibu na nyumba ya bondia huyo aliona nazi 6 zikiwa barabarani wakati anataka kuziokota ndipo alipotokea Mtuhumiwa (Mwakinyo) akiwa na kijana wake baada ya kumhoji walimpeleka ndani ya geti la nyumba na kufungulia Mbwa 6 ambao walianza kumshambulia.
Post A Comment: