Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wilayani Longido imeadhimisha Siku ya Afya ya Kinywa na Meno kwa kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Kimokowa juu ya umuhimu wa kutunza afya ya meno na kinywa.
Maadhimisho hayo yalihusisha utoaji wa elimu kupitia maigizo pamoja na mafunzo ya vitendo, huku wanafunzi na walimu wakipatiwa miswaki na dawa za meno ili kuwahamasisha kudumisha usafi wa kinywa.
Shirika la Ace Africa liliungana na idara hiyo katika kuadhimisha siku hii, likitoa mchango wake katika juhudi za kuelimisha jamii kuhusu afya ya kinywa. Utoaji wa elimu uliongozwa na Dr. Victor Ndale Mratibu wa Kinywa na Meno wa Wilaya ya Longido, ambaye alisisitiza umuhimu wa matunzo bora ya meno kwa afya bora ya mwili kwa ujumla.
“Tunawahimiza wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanadumisha usafi wa kinywa kwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku, kutumia dawa sahihi za meno na kuepuka vyakula vinavyoharibu meno,” alisema Dr. Ndale.
Maadhimisho haya yanalenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya kinywa na meno, huku mamlaka zikihimiza jamii kufanya uchunguzi wa meno mara kwa mara na kuzingatia lishe bora ili kuzuia magonjwa ya meno.
Post A Comment: