Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha pamoja na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuanzisha ushirikiano katika mafunzo ambayo yatalenga kuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa maadili na uwajibikaji wa viongozi wa umma yanakuwa dhahiri na yanaimarishwa kupitia elimu na utafiti. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano huo, Simbachawene amesema kuwa Mpango wa Taifa dhidi ya Rushwa na Kukuza Uadilifu ni dhihirisho la dhamira ya serikali katika kuhakikisha tunajenga jamii yenye maadili, uwajibikaji, na uwazi.

 Aidha, ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza mara kwa mara kuwa "Mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kuwa kazi ya mtu mmoja au taasisi moja; ni jukumu letu sote kama Taifa. Hivyo,  nazipongeza kwa dhati hizi taasisi mbili". 

Mkuu wa Chuo IAA  Prof. Eliamani Sedoyeka  ameeleza kuwa, Elimu bila maadili ni hatari, na maadili bila elimu ni bure. Amesema kuwa, kauli hiyo inaakisi umuhimu wa kuunganisha elimu ya kitaaluma na maadili thabiti katika uongozi. Taasisi za elimu ya juu zina wajibu wa kuhakikisha kuwa wanaowazalisha wanakuwa si tu wataalamu wa fani zao, bali pia viongozi wenye maadili mema na wenye kuzingatia misingi ya utawala bora.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo Prof. Sedoyeka amesema makubaliano hayo na Sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa Umma yamejikita katika kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali katika jamii. 

Pia, Prof. Sedoyeka, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuweka msisitizo katika kukuza maadili ya viongozi wa umma huku akisema kuwa anaamini kwa pamoja, tutaweza kujenga Tanzania yenye utawala bora na maendeleo endelevu.

Naye Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesii amesema  Maadili na uongozi bora ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo taasisi za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia, na mashirika ya kimataifa.

Mhe. Jaji (Mst) Mwangesi amesisitiza kuwa, kupitia ushirikiano huo wataweza kujenga mfumo imara wa maadili unaozingatia misingi ya haki, usawa, na utawala bora.














Share To:

Post A Comment: