NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

TAASISI ya HakiElimu pamoja na Asasi zingine za Kiraia wameiomba Serikali kuchukua hatua za kukomesha matumizi ya adhabu za viboko shuleni na kuhimiza adhabu chanya/adhabu mbadala ambazo sio za kikatili ambazo zitahimiza nidhamu kwa wanafunzi.

Wito huo umetolewa leo Machi 6, 2025 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dkt. John Kalage mara baada ya kupata taarifa kifo cha mwafunzi kilichosababishwa na adhabu ya viboko iliyotolewa na mwalimu wake Februari 26, 2025 mkoani Simiyu.

Adhabu hiyo iliyopelekea kifo cha mwanafunzi aliyekuwa anaitwa Mhoja Maduhu wa kidato cha pili kutoka katika Shule ya Sekondari Mwasamba, Kata ya Lutubiga, Wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu.

Dkt. Kalage amesema Serikali inapaswa kutumia fursa ya mchakato wa mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 unaoendelea hivi sasa kuweka vipengele vya kuzuia matumizi ya viboko shuleni na adhabu zingine zinazotoa mwanya kwa walimu kufanya ukatili kwa wanafunzi.

"Kunatakiwa kuwekwa kwa sheria ya kupiga marufuku viboko, itasaidia kuzuia walimu kutumia adhabu hizi, na hivyo kupunguza na kuondoa kabisa ukatili kwa wanafunzi shuleni". Amesema

Aidha amesema kuwa Serikali inapaswa kuweka mpango wa utekelezaji ahadi iliyoiweka katika Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Dunia kuhusu kutokomeza ukatili dhidi ya watoto uliofanyika Bogotá, Colombia mnamo Novemba 2024, wa kuanzisha Madawati ya Ulinzi wa Watoto katika shule zote 26,659 ifikapo mwaka 2029.

"Madawati haya yatatoa mfumo rasmi wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya watoto wanaokumbwa na ukatili wa aina mbalimbali shuleni, ikiwa ni pamoja na vipigo, unyanyasaji wa kijinsia, na manyanyaso ya kisaikolojia". Amesema Dkt. Kalage.

Kwa upande wake, Meneja wa Mpango wa Watoto wa Children in Crossfire, Saraphina Lelo, amesema umuhimu wa kutumia mbinu za nidhamu zenye huruma zaidi kwa wanafunzi na kuwataka watunga sera kutambua madhara ya muda mrefu yanayosababishwa na adhabu ya viboko.

"Tunapendekeza matumizi ya mbinu zisizo za ukatili ambazo zinajenga tabia njema kwa watoto badala ya kuwaingiza katika hofu. Adhabu ya viboko huathiri si tu afya yao ya kiakili na kihisia, bali pia huathiri uwezo wao wa kujifunza kwa ufanisi,". Amesema

HakiElimu imeungana na Asasi za Kiraia ambazo ni vinara wa upingaji ukatili kwa watoto ikiwemo adhabu za kikatili shuleni ambao ni Save the Children, Msichana Initiative, TCRF, CiC, Shule Direct na Children in Cross Fire kupinga matukio kama hayo.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: