NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Katika jitihada zake za kuimarisha utunzaji wa mazingira na kukuza elimu ya uhifadhi wa taka kwa wanafunzi wa shule za msingi, Taasisi ya GSM Foundation imetoa msaada wa vifaa vya kuhifadhia taka kwa Shule ya Msingi Bwawani,Kata ya Kijichi, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na usimikaji wa mapipa 12 ya kuhifadhia taka kwa matumizi ya nje ya madarasa, vipipa taka 25 vya ndani ya madarasa, toroli moja la usafirishaji wa taka na kubandika mabango 50 yenye jumbe za kimazingira kwenye mazingira ya shule.
Mpango huu ni sehemu ya dhamira ya GSM Foundation ya kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kimkakati wa Hifadhi ya Mazingira wa mwaka 2022-2032, (National Environmental Master Plan for Strategic Interventions 2022–2032) na Sera ya Taifa ya Mazingira (2021) yenye malengo ya uboreshaji na usimamizi wa taka na mazingira nchini.
Akizungumza leo Machi 21, 2025 Jijini Dar es Salaam, wakati wa makabidhiano hayo, Mratibu wa Mradi, GSM Foundation, Julius Ndyakoha amesema mpaka sasa wameshafikia shule tano ambapo wamegusa wanafunzi zaidi ya elfu 20 na walimu zaidi ya 500 katika Wilaya ya Kinondoni na Temeke Jijini Dar es Salaam.
"Huu ni mwendelezo wa matukio yetu ambayo tumekuwa tukiyafanya kuifikia jamii kwa kushirikiana na wadau wengine". Amesema
Aidha amesema kuwa katika kuadhimisha Siku ya Misitu Tanzania, wametumia maadhimisho hayo kuhamasisha wanafunzi kuweza kupanda miti kama namna moja wapo ya kuweza kuepukana na athari za kimazingira ikiwemo pia suala la ukusanyaji wa taka.
Nae Afisa Elimu Kata ya Kijichi Mwakilishi wa afisa elimu ni Hurry Shomari ambaye amemuwakilisha Mratibu wa Elimu, ameipongeza Taasisi ya GSM Foundation kwa kuweza kufika na kukabidhi vifaa hivyo kwa moja ya shule za msingi zilizopo katika Kata ya Kijichi wilayani Temeke, hivyo wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika masuala ya maendeleo.
Amesema vifaa hivyo vitatumika kwa matumizi sahihi ili kuleta tija ya kukidhi yale GSM Foundation wamekusudia katika utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bwawani, Jamali Fakihi amesema uwepo wa vifaa hivyo utaifanya shule hiyo kuwa kinara wa usafi katika Manispaa ya Temeke.
Ameeleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia wanafunzi kujua umuhimu wa usafi wanapokuwa katika maeneo ya shuleni na majumbani kwao.
Pamoja na hayo, GSM Foundation imeandaa na kutoa mafunzo maalum yanayohusu elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi wa kike wawapo katika mazingira nje ya shule.
Kupitia mpango huo, GSM Foundation pia imetoa jumla ya box za taulo za kike 100 ambazo unaweza kutumia zaidi ya mara moja (Re-usable) ili kuwapunguzia wanafunzi na wazazi gharama za mara kwa mara kununua taulo izo.
Taasisi ya GSM Foundation imepanga kuendeleza juhudi hizo za kutoa elimu ya mazingira, elimu ya afya kwa wanafunzi wa kike na vifaa saidizi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira na kiafya. Wanalenga kuwawezesha wanafunzi wote kutimiza malengo yao ya kitaaluma bira ya kuwa na vikwazo vyovyote na kwa usawa.
Post A Comment: