Na. Peter Haule, Serengeti, Mara.

 
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, Bw. Victor Charles, amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuhudhuria katika mafunzo ya elimu ya fedha ili iweze kuwasaidia namna ya kukopa kwa ikiwemo inayotolewa na Halmashauri  kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.
 
Akizungumza alipotembelewa na Timu ya Wataalam wa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha ikiongozwa na Bw. Salim Khalfan Kimaro ili kujitambulisha, Bw. Charles alisema ni vema wananchi wakajitokeza kwenye mafunzo ili kupata uelewa wa namna ya kurejesha mikopo na mambo mengine.
 
Bw. Charles alisema kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wamefanyakazi kubwa ya kuunda vikundi na kuvifuatilia, lakini urejeshaji wa mikopo ni changamoto kubwa kutokana na mitazamo hasi ya mikopo inayotolewa na Serikali kwa watu wengi kukosa elimu ya fedha.
 
Alisema wapo wanaoamini mikopo ni misaada na baadhi ya wanufaika wa mikopo wenye mahitaji maalumu wanasema hawawezi kurejesha mikopo kutokana na ulemavu jambo ambalo linaleta changamoto kwa wengine wanaosubiri urejeshwaji wa mikopo ili na wao wanufaike.
 
“Niwaase wakazi wa Serengeti kuhudhuria mafunzo ya elimu ya fedha ambayo yanatolewa na wataalamu wabobezi kwa lengo la kuwasaidia kuondokana na changamoto za urejeshaji wa mikopo sambamba na uwekezaji wenye faida na kuweka akiba”, alisema Bw. Charles.
 
Alisema kwa upande wa Halmashauri, imejitahidi kutenga asilimia 10 kwa ajili ya mikopo kwa makundi ya wakina mama, vijana na wenye mahitaji maalum lakini changamoto ni utunzaji, utumiaji na kurejesha mikopo hiyo kutokana na kukosekana na elimu sahihi ya fedha.
 
Aidha Bw. Charles alisikitika kuwaona watu wanatembea na fedha mfukoni na kutafuta watakao wakopesha kwa riba wanazopanga wao huku wakijinadi kudai mikopo bila kutumia nguvu wakati wa urejeshaji jambo ambalo si kweli kwa kuwa wengi wamejikuta wakichukuliwa vyombo vyao vya ndani wanaposhindwa kurejesha kwa wakati.
 
Ameipongeza Wizara ya Fedha kwa hatua ya kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa itasaidia kuondoa changamoto zinazowakumba wananchi kwa sababu ya kukosa elimu sahihi ya masuala ya fedha.
 
“Wananchi wamekuwa wakipewa mikopo ikiwemo ya Halmashauri na wanaipokea bila kuwa na malengo na mwisho wa siku mikopo hiyo inachukuliwa kama sadaka ili hali ilitakiwa izalishe ili irudi na kuwanufaisha wengine”, aliongeza Bw. Charles.
 
Kwa upande wake kiongozi wa Timu ya Wataalam wa elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alisema kuwa wapo Wilayani hapo  kuwajengea  uelewa wananchi kuhusu usimamizi wa fedha, mikopo, uwekaji wa akiba, uwekezaji na masuala ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, elimu ambayo ikifanyiwa kazi inaondoa changamoto za kifedha.
 
Naye Daudi Peter Karioba, mkazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, alisema kuwa kumekuwa na matangazo mengi kuhusu uwekezaji jambo ambalo ni vigumu kujua eneo sahihi la kuwekeza, hivyo elimu ya fedha kuhusu uwekezaji imetoa mwanga wa wapi eneo sahihi la kuwekeza ili kupata faida hususani kwenye Hati Fungani za Serikali.
 
Alisema kuwekeza maeneo ambayo hayafahamiki vizuri ni tatizo kwa kuwa kunapotokea hasara ni vigumu kufidiwa au kuwa na njia mbadala ya kutatua changamoto iliyojitokeza
Share To:

Post A Comment: