Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema ndani ya miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan jumla ya shilingi Bilioni 3.4 zimetolewa na serikali kuu kwaajili ya fidia kwa wananchi mbalimbali waliopisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwenye ardhi walizokuwa wanazimiliki.
Mhe. Senyamule ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 17, 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya ardhi ya mwaka 1995, toleo la 2023, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pia kwa maelekezo yake na usimamizi wake ambao umesaidia pia kupata ufumbuzi wa kero za ardhi zaidi ya 24,000 zilizokuwa zikiwasumbua wananchi wa Mkoa wa Dodoma zikihusisha madai ya fidia, milki pandikizi na ucheleweshaji wa hati.
Akizungumzia Sera mpya ya ardhi inayozinduliwa leo na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Mjini Dodoma kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Mhe. Senyamule ameeleza kuwa kuzinduliwa kwa sera hiyo kutachangia kukuza kasj katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, upimaji wa ardhi na utoaji wa hati pamoja na kuongeza thamani ya ardhi.
Mhe. Senyamule amempongeza Rais Samia pia kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani Dodoma ikiwemo miradi ya miundombinu ya ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege pamoja na reli ya kisasa ya SGR, akisema maboresho hayo yamesaidia kuongeza thamani ya ardhi ya Dodoma kutokana na mahitaji ya ardhi kuongeza kwa watu mbalimbali kutaka kununua ardhi Mkoani humo.
Post A Comment: