Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amewatunuku vyeti vya ujuzi wafungwa 201 wanaoendelea kutumikia vifungo vyao gerezani, waliohitimu mafunzo ya fani mbalimbali yaliyotolewa na Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Bashungwa ametunuku vyeti hivyo leo, tarehe 11 Machi 2025, katika hafla ya uzinduzi wa programu ya urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo ya Jeshi la Magereza, iliyofanyika katika Gereza la Mtego wa Simba, Kingolwira mkoani Morogoro.
“Programu hii itatoa hamasa kwa wafungwa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za urekebishaji ili kupata ujuzi, elimu, na maarifa kwa ajili ya kuwasaidia kujiajiri au kuajiriwa pindi watakaporudi katika jamii baada ya kutumikia vifungo vyao magerezani, kwa kuwa watakuwa na vyeti vinavyotambulika na VETA,” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa ujuzi walioupata wakiwa gerezani utawawezesha kujiajiri, kupata kipato, kuondokana na tabia ya kurudia makosa, kupunguza uhalifu katika jamii, na kupunguza utegemezi kwa ndugu zao wanapotoka gerezani.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa ameliagiza Jeshi la Magereza kuendelea kutekeleza maono ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha programu za urekebishaji wa wafungwa ili kufikia matarajio yaliyokusudiwa ya kuleta hali ya amani na utulivu katika jamii.
Amewapongeza wafungwa waliotunukiwa vyeti na kuwasihi kuwa raia wema na kutii sheria baada ya kumaliza vifungo vyao. Pia ametoa rai kwa wafungwa walioko gerezani kuongeza juhudi katika ushiriki wa programu za urekebishaji zitakazowawezesha kupata ujuzi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameipongeza serikali kwa kuanzisha programu ya kurasimisha na kuwapatia taaluma na ujuzi wafungwa wakiwa gerezani.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu, amesema kuwa kutokana na mahitaji na mabadiliko, Jeshi la Magereza limekamilisha mitaala ya mafunzo kwa watumishi ili kuwajengea uwezo katika majukumu yao.
Awali, Mkuu wa Sehemu ya Viwanda wa Jeshi la Magereza, SACP Dkt. Uswege Mwakahesya, ameeleza kuwa jumla ya wafungwa 201 wanaume 151 na wanawake 50 wametunukiwa vyeti katika fani za ujenzi, ufundi magari, uundaji na uchomeleaji, umeme wa majumbani, upishi, useremala, ubunifu na ushonaji nguo, na ufundi bomba.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi itaendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza kuhakikisha Watanzania wanapata ujuzi mbalimbali.
Post A Comment: