Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema, ujenzi wa Viwanda vinne vya Uchenjuaji Madini ya Shaba ikiwemo kiwanda cha Shengde Precious Metal Resources Co. Limited kinachoendelea kujengwa katika eneo la Mahungu Kata ya Nala Jijini Dodoma vinatarajiwa kuwa mkombozi wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Shaba nchini.

Waziri Mavunde amebainisha hayo leo Februari 16, 2025 baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho na kutoa pongezi kwa Kampuni ya Shengde Precious Metal Resources Co. Limited kwa uwamuzi wa kujenga kiwanda hicho Jijini Dodoma .

Aidha, Waziri Mavunde amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamilia kwa dhati kuyaongezea thamani madini hapa hapa nchini ili kukuza ajira kwa watanzania na kuongeza Pato la Taifa ambapo amewaahidi kupatiwa ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini.

Pamoja na mambo mengine, Waziri wa Mavunde amewataka Wamiliki wa kiwanda hicho kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati ili kiweze kuanza uzalishaji kwa lengo la kuongeza tija katika Sekta ya Madini ikiwemo kuongeza ajira kwa watanzania, kipato kwa Wamiliki na kuongeza Pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali.

Pia, Waziri Mavunde amesema, kwa kipindi kirefu wafanyabiashara wa Madini ya Shaba wamekuwa wakisafirisha Madini yao kwenda kuuza umbali mrefu ambapo viwanda vinapatikana huku miundombinu ya usafirishaji malighafi hizo ikiwa na changamopo hivyo, viwanda hivyo vitakuwa suluhisho la changamato za usafirishaji na masoko kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini hayo.

Pia, Waziri Mavunde amesema, Serikali inatambua mchango wa Wachimbaji Wadogo wa Madini na kupelekea kutenga maeneo yenye taarifa za uwepo wa madini ili kuchimba kwa tija ambapo amesema Rais Samia ametoa Mashine za uchorongaji kwa ajili ya kuwafanyia Utafiti wachimbaji wadogo ili kuachana na uchimbaji wa kubahatisha na kuelekeza kuwa Wachimbaji Wadogo wanachangia zaidi ya asilimia 40 kwenye Pato la Taifa litokanalo na Madini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na Madini ya aina mbalimbali ambao unaongoza kwa uwepo wa aina nyingi za madini kuliko Mkoa wowote Tanzania na kuahidi kutenga eneo kubwa kwa ajili ya viwanda vya uongezaji thamani madini ili kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha uongezaji thamani madini nchini.

Aidha, Senyamule amempongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini ambapo amesema Mkoa huo una vipaumbele vitano ikiwa Madini ni moja ya kipaumbele cha Mkoa huo.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo alianza kwa kuipongeza Kampuni hiyo kwa uwamuzi wa kujenga kiwanda hicho Jijini Dodoma na alipata fursa ya kutoa utabulisho wa washiriki walioambatana na Waziri wa Madini katika ukaguzi wa shughuli hiyo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kawanda hicho Abia Mafia ameiomba Wizara ya Madini kupatiwa maeneo yenye taarifa za uwepo wa madini ya Shaba kwa wingi ili kupata malighafi za kutosha katika uendeshaji wa kiwanda hicho.

Aidha, Mafia amesema, pamoja na juhudi za Serikali kuwezesha uongezaji thamani madini ufanyike hapa hapa nchini lakini bado kuna changamato ya usafirishaji wa malighafi kutoka migodini mpaka kiwandani na ameiomba kuondolewa kwa baadhi ya tozo katika uchenjuaji wa madini ya Shaba.

Pamoja na mambo mengine, Mafia amesema mpaka sasa ujenzi wa Kiwanda hicho umegharimu zaidi ya bilioni 3 ambapo kiwanda kinatarajiwa kuanza uzalishaji mapema ifikapo Juni, 2025.








Share To:

Post A Comment: