Na. Eva Ngowi, WF, KILIMANJARO
Serikali imewaasa wananchi kuepuka kukopa fedha kwenye Taasisi ama vikundi vinavyotoa huduma za kifedha bila kusajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka athari zinazoambatana na mikopo umiza.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Vijijini Bw. Shadrack Mhagama, katika kikao kilichofanyika ofisini kwake alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha walioko Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Moshi Vijijini kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi.
Aidha, Bw. Mhagama aliwaasa wananchi wa Manispaa ya Moshi Vijijini hasa watoa huduma za fedha kuwa wahakikishe wanasajili biashara zao ili kuepuka kuwaumiza wananchi na mikopo kausha damu, na kuwataka pia wananchi waache kukimbilia huduma za haraka ambazo sio salama na kuwashauri kuwa kabla ya kuomba mkopo wahakikishe kuwa mkopeshaji yuko kihalali kwa mujibu wa sheria.
“Ni kweli kwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi tunao watu ambao wanatoa huduma za kifedha lakini hawajasajiliwa; kwa kweli tunaweza kusema ni biashara haramu (illegal business) ambayo inafanywa nje ya utaratibu. Pia imebainika kuwa wananchi wengi wako katika vikundi ambavyo havijasajiliwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, kwa hiyo nitoe rai kwa wananchi ni vyema wakawa na mwamko wa kujiunga katika vikundi ambavyo ni rasmi na vimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria hiyo.” Alisema Bw. Mhagama
Vilevile, Bw. Mhagama alitoa rai kwa wananchi kwa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika watoe taarifa kwa Mamlaka husika ambazo ni pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye Mamlaka zao za Wilaya na Mikoa, watakapobaini kuna vikundi vya huduma ndogo ya fedha mitaani vinatoa Huduma za Fedha pasipo kusajiliwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionensia Mjema alisema kuwa Serikali inaendelea na program ya utoaji elimu hapa nchini na kwa sasa ni zamu ya Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo wananchi wamepata elimu namna wanavyoweza kuwa na nidhamu ya kujiwekea akiba lakini pia wamepata uelewa juu ya mikopo umiza ili kuepukana na changamoto hiyo kwa sasa ya mikopo kausha damu.
Awali, akizungumza katika semina hiyo Mkazi wa Kata ya Uru Mashariki, Halmashauri ya Moshi Vijijini, Bi. Lusiana Mushi, alisema kuwa ujio wa Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha umewafungua macho kuhusiana na akiba, vyama viwe vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na sehemu salama ya kuweka fedha.
Aidha, Bw. Philbert Macha ambaye pia ni mwana kikundi kilichopo katika Kata ya Mbokomu, Halmashauri ya Moshi Manispaa alisema kuwa kupitia elimu aliyoipata amejifunza mengi na ataenda kuwaelimisha watu wengine maana anaona mikopo mingi inakopeshwa na watu binafsi na taasisi mbalimbali ambapo wengi wanakopa bila kuwa na malengo.
Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha imefanikiwa kutoa elimu ya fedha katika Shule ya Sekondari Mbokomu, Vikundi vya wakina mama na wajasiriamali wadogo wadogo Kata ya Mbokomu na Wanakijiji wa Kata ya Uru Mashariki, Halmashauri ya Moshi Manispaa Mkoa wa Kilimanjaro.
Post A Comment: