📍Azindua Mabasi ya kusafirisha Maabusu

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innnocent Bashungwa amelitaka Jeshi la Magereza kusimamia kikamilifu mpango wa kuwapa ujuzi na mafunzo ya ufundi stadi Wafungwa wanapokuwa Gerezani na watakaohitimu mafunzo kutunukiwa vyeti vinavyotambuliwa na VETA wakati wanapomaliza vifungo vyao ili kuwajengea uwezo kujitegemea wanaporudi katika jamii.

Bashungwa ameeleza hayo tarehe 14 Februari 2025 wakati alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Dodoma ambapo amebainisha kuwa Jeshi hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) litaanza utekelezaji wa mpango wa kuwapa mafunzo Wafungwa wanapokuwa Gerezani.

Bashungwa ameeleza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Jeshi la Magereza wa kuwapo ujuzi wa ufundi stadi Wafungwa wanapokuwa wanatumikia vifungo yao pamoja kurasimisha ujuzi wanakuwa nao na kuwapatia vyeti.

“Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, kuwapa ujuzi (ufundi stadi) kwa kuwaendeleza wanaoingia gerezani na ujuzi, lakini wale wanaoingia hawana ujuzi kabisa, kuangalia namna ya kuwapa ujuzi ili wanapotokaa waweze  kujikimu kimaisha” ameeleza Bashungwa 
 
Aidha, Bashungwa amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliboresha Jeshi la Magereza kwa kulipatia vifaa na vitendea kazi ikiwa ni pamoja na Mabasi saba ya kusafirisha maabusu ambayo ameyazindua.

Bashungwa baada ya kuzindua Mabasi ya kusafirisha Maabusu, amemtaka Kamishna Jenerali wa Magereza CGP Jeremiah Katungu na Menejimenti kusimamia na kutunza mabasi saba aliyozidua ili yaweze kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Kadhalika, Bashungwa ameeleza kuwa Jeshi la Magereza limekuwa mstari wa mbele kutumia nishati safi ambapo hadi sasa Magereza yote nchini yanatumia nishati safi na salama ya kupikia wakati wa kuandaa chakula cha Wafungwa.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza CGP Jeremiah Katungu ameishukuru Serikali kwa kuliwezesha Jeshi la Magereza kununua magari mapya ikiwa pamoja ya Mabasi ya kusafirisha maabusu kutoka Gerezani kwenda Mahakamani ili kuwasaidia watuhumiwa kesi zao kusikilizwa na haki kutendeka kwa wakati.
Share To:

Post A Comment: