Na Fredy Mgunda, Lindi.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Lindi kimeadhimisha miaka 48 tangu kuanzishwa kwake kwa njia ya kipekee, kwa kukata keki kuashiria mafanikio ya chama hicho tangu kilipoanzishwa hadi sasa, kikiwa chama tawala nchini Tanzania.
Katika maadhimisho hayo, wadau mbalimbali mkoa wa Lindi wameonyesha kuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, na kumtaja kama kiongozi ambaye ameleta maendeleo makubwa na amani kwa wananchi. Kulingana na Kulusumu Lunje, ambaye ni mmoja wa wanaharakati wa mkoa wa Lindi, wanawake wa mkoa huo wana imani kubwa na Rais Samia, huku wakisema kuwa maendeleo anayoleta katika kila wilaya ni ya manufaa kwao na jamii kwa ujumla.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Lindi, Patrick Magarinja, alisisitiza kuwa Rais Samia ameboresha maisha ya wananchi wa Lindi kwa muda mfupi alioingia madarakani.
Magarinja aliongeza kuwa maendeleo yaliyoshuhudiwa mkoa wa Lindi ni ishara ya utendaji kazi mzuri wa serikali inayoongozwa na Rais Samia.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, alieleza kuwa serikali ya mkoa huo imejipanga vilivyo kuhakikisha kwamba Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 inatekelezwa kwa vitendo.
Moyo alisisitiza kuwa hakuna mtumishi wa umma atakayeruhusiwa kushindwa kutekeleza majukumu yake, na kuwa lazima wafanyakazi wa serikali watimize wajibu wao katika kuhakikisha mafanikio ya serikali yanatimia.
Moyo alikumbusha kuwa CCM ndio waliosaidia kuuweka madarakani utawala wa Rais Samia, na kwa hiyo, ni jukumu la kila mtumishi wa umma kuhakikisha kwamba anatekeleza majukumu yake kikamilifu.
Hii ni kuhakikisha kuwa malengo ya chama yanafanikiwa, na mkoa wa Lindi unazidi kupiga hatua kimaendeleo.
Kwa ujumla, maadhimisho hayo ya CCM mkoa wa Lindi yamekuwa ni platform muhimu ya kuonyesha mshikamano na kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, huku wadau wakieleza matumaini yao ya maendeleo zaidi katika miaka ijayo.
Post A Comment: