WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wataalamu wa wizara hiyo kutumia Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika mkoani Singida kubuni njia zitakapunguza foleni mijini na kuongeza mapato ya serikali. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Baraza hilo, Waziri Ulega alisema pamoja na mkutano huo kuwa na ajenda zake za kawaida kisheria, ni muhimu masuala muhimu kama ya foleni ambayo yanagusa wananchi wengi yakajadiliwa kwa kina kwa sababu mkutano huo umesheheni wataalamu wa kutosha. 

Akizungumza kwa mifano, Ulega alisema binafsi anaona fursa ya kupunguza kero ya foleni na serikali kujiongezea mapato endapo ubunifu utafanywa kwenye maeneo ambako kuna barabara za mwendokasi. 

"Hivi hakuna namna ambayo kwa kulipia, magari ya kawaida yanaweza kutumia njia ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) endapo njia za kawaida zitakuwa na foleni? Kwa nini barabara moja ikae nusu saa bila gari kupita wakati kwingine hakuendeki kwa sababu ya foleni? 

"Kwenye daraja la Mwalimu Nyerere tunafanya hivyo tayari kwa PPP na watu wanalipa kuvuka daraja. Nchi nyingine watu wanalipia kutumia baadhi ya barabara kama hawataki foleni. Naamini tunaweza kufanya kitu lakini tunahitaji wataalamu mtushauri," alisema Ulega.

Katika hatua nyingine, Ulega amewaagiza watumishi wa Wizara ya Ujenzi kuhakikisha wanazingatia thamani ya fedha wakati wa utekelezaji na usimamizi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo barabara, madaraja, vivuko, majengo ya Serikali na viwanja vya ndege. 

“Nawaelekeza  muendelee kuunga mkono dhamira hii njema ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwenye miradi mnayoisimamia”, amesema Ulega

Aidha, Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuongeza juhudi za usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya dharura ya miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua El-Nino na Kimbunga Hidaya yenye thamani ya Shilingi takriban bilioni 868.56.

Ameelekeza Viongozi wa Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kuhakikisha kuwa dhana ya uwezeshaji wa Makandarasi wa ndani inatekelezwa kama ilivyokusudiwa ili kunufaisha na kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kuufungua mkoa wa Singida  kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami ambazo zimesaidia kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji  katika mkoa huo.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza hilo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi, Aisha Amour amesema kuwa Wizara inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi na ujenzi wa daraja la Mwendokasi (BRT) jijini Dar es Salaam.  

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi umefanyika mkoani Singida ambapo ajenda kuu katika Mkutano huo ni kupokea, kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwakawa fedha 2025/26 kabla ya Bajeti hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushirikisha wajumbe mbalimbali kutoka Wizarani na Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.

Share To:

Post A Comment: