Na Denis Chambi, Tanga.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania 'TRA' Mkoa wa Tanga imeendelea kufanya vizuri kwa mara ya Saba mfululizo katika ukusanyaji wake wa mapato hii ikiwa ni baada ya kuvuka lengo lake katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Mamlaka hiyo ambayo kwa kipindi cha kutoka July 2024 hadi January 2025 iliwekewa lengo la kukusanya kiasi cha Bilioni 191 imevuka lengo na kufikisha ukusanyaji wa Bilion 200 fedha ambayo ni makusanyo ya mwaka mzima wa fedha uliopita wa 2023/2024.
Akizungumza katika hafla maalum ya kuwapongeza na kutoa vyeti kwa walipa kodi waliofanya vizuri meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzani mkoa wa Tanga Thomas Masese amesema kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano mkubwa baina yao na wafanyabiashara kwa kuwapa elimu ya ulipaji wa kodi kwa hiari hatua ambayo imewawezesha kufikia ongezeko la asilimia 76.
"Lengo letu la mwaka huu ni kukusanya Bilion 335 kati ya hizo Bilion 77 ni kodi za ndani na Bilion 257 ni kodi za Forodha, hadi sasa tuna miezi saba tulikuwa na lengo la kukusanya bilioni 191 lakini tumekusanya Bilion 200 sawa na ufanisi wa asilimia 105"
"Lakini katika kipindi hiki cha miezi saba kutoka July 2024 mpaka January 25 ukilinganisha na mwaka uliopita kuna ongezeko la asilimia 76 mpaka sasa ukilinganisha kiasi tulichokusanya bilion 200 inakaribiana kabisa na kiwango tulichokusanya mwaka mzima wa jana ambapo tulikusanya Bilion 204 lakini mpaka sasa tumeshavuka lengo" alisema
Aidha Masese amesema kuwa ipo mikakati mbalimbali waliyojiwekea ili kuendelea kuwa kinara wa ukusanyaji wa mapato ukilinganisha na mikoa mingine Tanzania ambapo wamejipanga kuimarisha mahusiano na walipa kodi, kusikilizia na kutatua changamoto zote za wafanyabiashara, kuendelea kutoa elimu ya ulipaji kodi kwa hiari, kuendelea kupambana na upotevu mapato ikiwemo matumizi sahihi ya mashine za elektroniki "EFD mashine pamoja na kuimarisha doria za mipakani kwa kuzuia magendo.
Akizungumza mara baada ya kugawa tuzo hizo kwa wafanyabiashara Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani ameipongeza mamlaka ya mapato Tanga kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wake huku akiwataka kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kujua umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari.
"Nchi nyingi duniani zinategemea jodi ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wake na sisi kama miongoni mwa nchi hizo tunaendelea kutegemea kodi ili kutengeneza mipango mbalimbali ya maendeleo kwahiyo ni watanzania wenyewe tunaiwezesha nchi yetu kutulete maendelo niwapongeze sana ndugu zetu wa TRA kwa ufanisi huu wa makusanyo." Alisema
Dk Buriani amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara kote nchini ili kuwa na uwezo wa kulipa kodi bila shurti sambamba na kuweka mazingira rafiki kwaajili ya wawekezaji wa ndani na nje ili kuweza kutanua wigo wa kujiongezea mapato.
"Serikali itaendelea kuweka msisitizo na mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ili kuendelea kuwapa uwezo wa kulipa kodi kwa hiari, kuwatambua wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa lakini vilevile wawekezaji ili kuongeza mapato kukuza ajira na kuondoa umasikini" alisema Dkt. Buriani.
Aidha amewataka wafanyabiashara kuitumia bandari ya Tanga ambayo imefanyiwa maboresho makubwa ya zaidi ya shilingi Bilion 429 kutuma na kupokea mizigo ambapo Meli kubwa zinatia nanga tofauti na awali huku akiwaasa kujiepusha masuala ya kukiuka sheria ya ulipaji wa kodi.
Amewataka watumishi wa TRA Mkoa wa Tanga kuendelea kuwa waadilifu na kuzingatia maadili yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kupambana na upotevu wa mapato kuziba mianya ya rushwa.
"Ni lazima kulinda mapato ya Serikali kwa kodi zetu kuhakikisha kwamba tunaziba mianya yote ya rushwa kwa kuzingatia maadili msiruhusu watu wachache wakanufaika na wengi wanakosa haki"alisisitiza Dkt Buriani
Katibu wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania "JWT" Mkoa wa Tanga Ismail Masoud ameishukuru na kupongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara hususani wajasiriamali wadogo wadogo hatua ambayo imewahamasisha wengi kulipa kodi bila shurti.
"Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania kauli mbiu yetu tunasema tulipe kodi kwa hiari tuijenge nchi yetu, Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan anatusaidia sana wafanyabiashara tukuze mitaji yetu tunanufaika sana na sasa tunalipa kodi kwa hiari mpaka tunavuka malengo" alisema Masoud.
Post A Comment: