Wataalamu wa misitu, wanasayansi, na wahifadhi wa mbegu za miti kutoka Tanzania, Kenya, Italia, na Uingereza wamekutana jijini Dodoma kwa mkutano wa siku tano kujadili urejeshaji na matumizi endelevu ya miti asili ya Tanzania.
Mkutano huu ni sehemu ya mradi wa Kuongeza upatikanaji wa aina mbalimbali za Mbegu za miti ya Asili Tanzania kwa Ajili ya Watu na Bioanuwai, unaofadhiliwa na Mpango wa Darwin wa Uingereza na kusimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Washirika wa mradi huu ni taasisi za uhifadhi zikiwemo Botanical Garden Conservation International (BGCI), Bustani ya Mimea ya Migombani (Zanzibar), Taasisi ya ECHO East Africa (Arusha), Umoja wa Vikundi vya Upandaji Miti Tanzania (TTGAU), na Kamati ya Mashauriano ya Wauzaji wa Mbegu na Miche ya Miti (SSCG).
Mkutano huu unalenga kusaidia juhudi za Tanzania katika kutimiza ahadi yake ya kurejesha hekta milioni 5.2 za ardhi iliyoharibika ifikapo mwaka 2030 kupitia Mpango wa Bonn (Bonn Challenge) na mpango wa Afrika (AFR100). Tanzania ina aina 1,755 za miti asili, lakini nyingi zinakabiliwa na tishio la kutoweka kutokana na uvunaji holela na matumizi yasiyoendelevu.
Katika siku tatu za kwanza, wataalamu watashiriki warsha maalum ya kuchagua aina 100 za miti asili yenye umuhimu mkubwa kiikolojia na kiuchumi.
“Tunachagua miti inayochangia kuhifadhi mazingira, bioanuwai, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, huku pia ikileta manufaa ya kiuchumi kwa jamii,” alisema SACC Fandey H. Mashimba, Mratibu wa Mradi kutoka TFS aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Siku mbili za mwisho zitahusisha mafunzo maalum ya wakufunzi (ToT) yakiongozwa na TFS na BGCI, ambapo washiriki zaidi ya 40 kutoka TFS, mashirika yasiyo ya kiserikali, wasimamizi wa vitalu vya miche, na wanajamii watapata ujuzi kuhusu ukusanyaji wa mbegu, uteuzi wa miti inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, na mifumo jumuishi ya biashara kwa jinsia zote.
“Hatulengi tu kupanda miti, bali tunapanda fursa za kiuchumi kwa jamii,” alisema Roniance Adhiambo, Meneja wa Miradi wa BGCI Kanda ya Afrika Mashariki.
Cristina Colleto, Mkuu wa Uhifadhi wa Miti kutoka BGCI, aliongeza: “Huu ni mradi unaoongozwa na Tanzania, lakini mafanikio yake yanategemea ushirikiano wa kimataifa.”
Kwa upande wake, Yvvete Harvey-Brown, Afisa Uhifadhi wa BGCI, alihimiza ushirikiano wa Watanzania na TFS ili kuhakikisha mafanikio ya mradi. “Jamii zina jukumu kubwa katika kulinda miti asili. Hizi si mizizi tu ya historia yetu, bali mbegu za mustakabali wa kizazi kijacho,” alisema.
Ifikapo mwaka 2026, mradi huu unatarajiwa kuhakikisha miti asili inakuwa sehemu ya mipango ya kitaifa ya urejeshaji misitu, huku pia ukitoa taarifa za kitaalamu kwa watunga sera ili kuimarisha matumizi endelevu ya mbegu za miti asili kwa manufaa ya mazingira na uchumi wa taifa.
Post A Comment: